MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga jana walianza vyema kampeni ya
kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0
mbele ya Coastal Union ya Tanga katika mchezo mkali uliofanyika kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Licha ya kuanza vyema mbio hizo za kutetea taji lake, lakini ushindi
huo umeipeleka Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo inayoshiriki timu
16 ikiongoza kwa wastani wa mabao huku nyavu zake zikiwa hazijatikiswa.
Yanga iliuanza mchezo huo kwa kasi na kupata bao la mapema la dakika
ya saba lililofungwa na mchezaji bora na mfungaji bora wa msimu
uliopita, Simon Msuva, akimalizia pasi nzuri ya Amissi Tambwe.
Bao hilo lilionekana kuwaongezea kasi Yanga ambao katika mchezo huo
iliwatumia wachezaji wake wa kimataifa kutoka Zimbabwe, Donald Ngoma na
kiungo Thaban Kamusoko, ambao huo ulikuwa mchezo wao wa kwanza kwenye
ligi ya Tanzania.
Baada ya kuona mambo magumu, kocha wa Coastal Union, Mganda Jackson
Mayanja alifanya mabadiliko ya mapema kwa kumtoa Adeyoum Saleh na
kumuingiza Twaha Ibrahim ambaye alisaidia kuituliza timu hiyo.
Mshambuliaji wa Coastal Union, Ali Ahmed Shiboli alijitahidi
kupambana katika kipindi cha kwanza ili angalau kuipatia timu yake bao
la kusawazisha, lakini walinzi Kelvin Yondani na Nadir Haroub walikuwa
makini kumdhibiti.
Wakati timu zikijiandaa kwenda mapumziko, Ngoma aliifungia Yanga bao
la pili dakika ya 42 na akimalizia mpira uliodondoka baada ya kugongwa
kwa kichwa na beki wa Coastal, Tumba Swedi aliyeruka na Tambwe kugombea
krosi ya Msuva.
Kipindi cha pili timu zote zilionekana kujipanga na Coastal Union
walionekana kupania kusawazisha mabao hayo, lakini walijikuta
wakinusurika kufungwa bao la tatu baada ya Tambwe kupoteza nafasi ya
wazi akiwa amebaki na nyavu baada ya mpira uliopigwa na Haruna Niyonzima
kumshinda kuumalizia wavuni.
Dakika ya 55, Shiboli alimpiga chenga Nadir na kubaki na kipa Ally
Mustapha, lakini shuti lake halikulenga lango. Mwishoni mwa kipindi cha
pili, Yanga ilimtoa Tambwe na nafasi yake kuchukuliwa na Malimi Busungu
ambaye alicheza vizuri na kupoteza nafasi mbili za wazi alizozipata sawa
na Dues Kaseke aliyeingia badala ya Geoffrey Mwashiuya.
Kwa ushindi huo, Yanga ina pointi tatu sawa na timu za Azam FC,
Mtibwa Sugar, Simba, Majimaji FC, Toto Africans na Kagera Sugar, lakini
ikiwa kileleni kwa kutofungwa bao lolote. Ligi hiyo itaendelea
keshokutwa.
Yanga: Mustafa, Mbuyu Twite, Mwinyi Haji Mngwali, Yondani, Nadir,
Kamusoko, Msuva, Niyonzima/ Salum Telela, Tambwe/Busungu, Donald Ngoma
na Mwashiuya/Kaseke.
Coastal Union; Sabwato Nicholas Godfrey Wambura/Mbwana Hamisi
‘Kibacha,’ Hamad Juma, Yassin Mustafa, Ernest Joseph Mwalupani, Swedi,
Said Jeilan/Patrick Protas, Shiboli, Youssoufa Sabo, Nassoro Kapama na
Adeyoum/Twaha. Yanga kileleni
0 comments:
Post a Comment