HELIKOPTA iliyobeba makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikitokea Dar
es Salaam kwenda Njombe imeanguka ndani ya Pori la Akiba la Selous
lililopo eneo la Kilombero mkoani Morogoro.
Akitoa taarifa za ajali hiyo kwa MTANZANIA jana, Meneja wa Selous,
Benson Kibonde, alisema helikopta hiyo ilianguka karibu na Mto Ruaha
katika Kitalu cha Uwindaji cha R3.
“Ajali hiyo imetokea jana jioni na tulipata taarifa kwa njia ya simu
ya satellite kutoka kwa professional hunter (mwindaji) mmoja ambaye
alisema akiwa katika hema lake ndani ya Pori la Selous katika Kitalu cha
R2 alisikia kishindo cha helikopta ikianguka na kutoa moshi katika
upande wa Kitalu cha R3,” alisema Kibonde.
Alisema baada ya ajali hiyo kutokea, mwindaji huyo pia alitoa taarifa
kwa Kampuni ya Uwindaji ya Foa Adventure ambayo imempeleka katika pori
hilo.
Alisema kutokana na eneo hilo kuwa karibu na Mto Ruaha ilikuwa ni vigumu kwao kwenda kwa kuwa usiku ulishaingia.
“Si rahisi kwenda eneo lile nyakati za usiku kwa sababu usiku
ulishaingia na kwa mazingira yalivyo ni vigumu na sisi tumeamua askari
wetu wa wanyamapori wataenda asubuhi katika eneo lilipotokea ajali
hiyo,” alisema Kibonde.
Hata hivyo, MTANZANIA lilipata taarifa kuwa miongoni mwa makada
waliokuwamo katika helikopta hiyo alikuwa ni mgombea ubunge wa Jimbo la
Ludewa kwa tiketi ya CCM, Deo Filikunjombe.
MTANZANIA lilimtafuta Mathias Luoga ambaye ni Msaidizi wa
Filikunjombe na alisema katika helikopta hiyo kulikuwa na abiria watatu
na rubani mmoja.
“Saa 10 jioni ya jana, Filikunjombe alikuwa anatokea Dar es Salaam
kwenda Njombe lakini wakiwa angani helikopta yao ikapata hitilafu wakiwa
eneo la Kilombero na kuanguka katika Mbuga ya Selous.
“Lakini eneo ilipoanguka helikopta hiyo hakuna mtandao wa simu
unaopatikana kwa hiyo mawasiliano yamekuwa magumu ndiyo maana
hawajapatikana na askari wanyamapori walisema watawatafuta,” alisema
Luoga.
Katika hatua nyingine, MTANZANIA lilimtafuta Filikunjombe kupitia
simu yake ya mkononi ambayo iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa kisha
baadaye haikupatikana.
0 comments:
Post a Comment