Muungano wa Ulaya EU umeanzisha
operesheni mpya ambayo itahusisha kuzuiwa kwa meli zinazowasafirisha
wahamiaji wanaotaka kufika Ulaya zikiwa kwenye bahari ya Mediterranean.
Chini
ya operesheni hiyo kwa jina Sophia inayoshirikisha meli sita za
kijeshi, wanajeshi wa majini watakuwa na ruhusa ya kuabiri meli,
kupekua, kukamata na kuelekeza kwingine meli zinazoshukiwa kutumiwa
kusafirisha watu.
Hadi sasa, EU ilikuwa imeangazia tu kufuatilia meli baharini na uokoaji.
Mwaka huu, zaidi ya wahamiaji 130,000 wameingia Ulaya kutoka Afrika kaskazini. Zaidi ya 2,700 wamekufa maji.
Hata
hivyo, wahamiaji wengi na wakimbizi, hasa wanaotoroka mapigano Syria,
wanafika Ulaya kwa kuvuka na kuingia Uturuki kwa miguu kabla ya kutumia
bahari kuingia Ugiriki ambayo ni mwanachama wa Muungano wa Ulaya. Wengi
wanataka kwenda Ujerumani.
Mzozo wa wahamiaji unatarajiwa kuwa
moja ya masuala makuu yatakayozungumziwa Chansela wa Ujerumani Angela
Merkel na Rais wa Ufaransa Francois Hollande watakapofanya hotuba nadra
ya pamoja kwa Bunge la Ulaya mjini Strasbourg baadaye Jumatano.
Mara
ya mwisho viongozi wa mataifa hayo kutoa hotuba kama hiyo ilikuwa 1989
wakati Francois Mitterrand alipokuwa akiongoza Ufaransa naye Helmut Kohl
Ujerumani.
Hata hivyo, kuna mambo ambayo operesheni hiyo ya EU
haitaweza kuyafanya. Meli za kivita lazima ziheshimu mipaka ya kimataifa
baharini, hii ikiwa na maana kwamba haziwezi kuingia eneo la maili 12
kutoka pwani ya Libya.
0 comments:
Post a Comment