RAIS Uhuru Kenyatta amesema nchi yake itakuwa mteja wa gesi ya
Tanzania mara itakapoanza kuuzwa nje baada ya uzinduzi unaotarajiwa
kufanyika Mtwara Jumamosi wiki hii. Aidha, amesema Kenya ina deni kubwa
kwa Rais Jakaya Kikwete kutokana na urafiki wao na uhusiano mkubwa kati
ya nchi hizo mbili.
Rais Uhuru aliyasema hayo juzi mjini hapa, wakati wa dhifa ya kitaifa
aliyomwandalia Rais Kikwete aliyekuwa hapa kwa ziara ya kiserikali ya
siku tatu. “Tumekuwa marafiki wa muda mrefu, leo tunajisikia furaha
kubwa kuagana na rafiki wa muda mrefu na mtu muhimu kwa Kenya.
Tunajivunia kuwa naye na tuna deni kutokana na uhusiano wetu mkubwa,”
Rais Uhuru alisema. Alimweleza Rais Kikwete kuwa, katika utawala wake,
alisimamia ajenda ya kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na biashara
kati ya Kenya na Tanzania ambayo alisema imefikia nusu kwa nusu.
“Katika utawala wako pia umesimamia sana masuala ya miundombinu ya
kuunganisha nchi zetu. Barabara ya Arusha – Athi uliyozindua na Rais
mstaafu Mwai Kibaki na ile ya juzi ya Voi – Arusha ambayo itaunganisha
na bandari ya Mombasa ni ushahidi tosha wa jinsi wa kuimarika kwa
biashara kati ya nchi zetu,” alieleza.
Kuhusu gesi ya Mtwara, Rais Uhuru alisema mapinduzi hayo mapya katika
maendeleo, pia yataisaidia Kenya kwani itapata nishati kwa bei rahisi
na inayoaminika. “Maendeleo mapya katika mradi wa gesi ni eneo jingine
ambalo Kenya itafaidika nalo, kwani tutanunua kwa bei rahisi na tutakuwa
na nishati inayoaminika na hivyo kusaidia kujenga nchi yetu kiuchumi na
kijamii.
“Asante sana kwa kazi nzuri,” alisema Rais Uhuru na kumtaja Rais
Kikwete kama rafiki wa kweli na mwana Afrika Mashariki mahiri. Rais
Kikwete anafahamika vizuri kwa Wakenya baada ya kusaidia kusuluhisha
mgogoro wa kisiasa mwaka 2007 uliosababishwa na matokeo ya uchaguzi mkuu
wa rais.
Aidha, Rais Uhuru alimweleza Rais Kikwete kuwa zipo changamoto
zinazozikabili nchi zote mbili ambazo ni ugaidi, ujangili na matumizi ya
dawa za kulevya ambazo alisema anaamini mrithi wa Kikwete ataendeleza
mapambano dhidi ya changamoto hizo.
Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema katika wiki chache zijazo,
watasimamia masuala hayo ili yanayowezekana sasa yafanyike haraka
ikiwamo kusaini makubaliano ya awali (MoU) kuhusu matumizi ya gesi
kutoka mkoani Mtwara.
Rais Kikwete alikuwa Kenya kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais
Uhuru Kenyetta ambapo aliitumia nafasi hiyo kuwaaga Wakenya na Jumuiya
ya Afrika Mashariki ambayo kwa sasa ni mwenyekiti wake.
0 comments:
Post a Comment