MSHAMBULIAJI wa Kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta amesema wapo
tayari kulaumiwa na mashabiki endapo watashindwa kuifunga Malawi leo.
Samatta aliyasema hayo jana baada ya mazoezi yaliyofanyika kwenye Uwanja
wa Taifa kujiandaa na mchezo wa leo dhidi ya Malawi wa kutafuta kufuzu
fainali za Kombe la Dunia 2018 zitakazofanyika Urusi.
“Mimi naamini Malawi ni wepesi kuliko Nigeria ambao tulitoka nao
suluhu hapa Taifa (Uwanja), hivyo mchezo wa kesho (leo) ushindi ni
muhimu na tusiposhinda mchezo huu nipo tayari kulaumiwa na mashabiki”,
alisema Samatta.
Pia Samatta alitolea ufafanuzi madai ya kuwa hachezi vyema kuisaidia
Taifa Stars na kusema siyo kweli kwamba anacheza vizuri akiwa na timu
yake ya TP Mazembe tofauti na akiwa Taifa Stars, bali inatokana na aina
ya wachezaji anaocheza nao.
“Sisemi kuwa Tanzania hakuna vipaji bali hii inatokana na wachezaji
ninaocheza nao na unaokutana nao kwa sababu kwenye timu ya taifa
tunafanya mazoezi muda mchache kuliko kwenye timu yangu ninayocheza
hivyo inasababisha kuonekana sichezi kwa kiwango kile ambacho ninacheza
nikiwa na TP Mazembe”, alisema Samatta.
Samatta ambaye anacheza TP Mazembe ambayo imefuzu fainali za klabu
bingwa Afrika amesema ana imani ataibuka kuwa mfungaji bora katika
mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya mpinzani wake timu
yake kutolewa.
Pia alisema ndoto yake ya kucheza soka Ulaya inakaribia kutimia kwani
Desemba mkataba wake na TP Mazembe unamalizika na anaamini hakuna
kitakachomzuia kwenda kucheza Ulaya.
“Mimi nina ndoto ya kucheza Ulaya na sifanyi hivyo kwa sababu ya
kipato kwani kama ni kipato nadhani hata TP Mazembe wanalipa vizuri
kuliko baadhi ya timu za Ulaya”, alisema Samatta.
0 comments:
Post a Comment