Kada mkongwe wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kingunge
Ngombale Mwiru ameanza rasmi kazi ya kupanda jukwaani kukizamisha chama
chake cha zamani baada ya kuwaambia wananchi wa Arusha kuwa wamchague
mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward
Lowassa ili aingie Ikulu baada ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
Kingunge aliyeitumikia CCM kwa miaka zaidi ya 60 kabla ya kukihama
wiki iliyopita kwa madai kadhaa yakiwamo ya kupuuzwa misingi ya
kuanzishwa kwake, aliwaambia maelfu ya wananchi waliojitokeza kwenye
viwanja vya Sinon, Unga Limited mjini hapa kuwa Lowassa ndiye mgombea
mwenye sifa zote za uongozi na hivyo, wanapaswa kuungana na Watanzania
wengine katika kumpigia kura nyingi za ndiyo ili kuing’oa CCM
madarakani.
Alisema kwa kufanya hivyo, ndipo Watanzania watakuwa na fursa ya
kutoa nafasi ya kufanyika kwa mabadiliko ya kweli ya uongozi kwa manufa
ya taifa.
Kadhalika, aliwataka wananchi kuchagua pia wagombea wa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, Chama cha
Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD ili kuiondoa kabisa CCM katika kila
ngazi. Mbali na kupeperusha bendera ya Chadema, Lowassa pia anawakilisha
Ukawa.
“Mnapofika kwenye vituo vya kupigia kura, mchagueni Lowassa... na
pia wabunge na madiwani wa Ukawa,” alisema na kuibua shangwe kubwa
kutoka kwa watu waliojitokeza kwenye mkutano huo.
Akieleza zaidi, Kingunge alirudia kauli yake aliyoitoa wiki
iliyopita wakati akitangaza kujiondoa CCM kwa kusema kuwa chama chake
hicho cha zamani kimeshaishiwa pumzi na hivyo hakina tena uwezo wa
kuiongoza Tanzania, ushahidi ukiwa ni kushindwa kwake kuinua uchumi.
“CCM pumzi imekwisha. Wale wenye pumzi ndiyo watakaoweza kufika
kileleni... tunahitaji mabadiliko ili tuweze kupambana na umasikini na
kuinua uchumi kwa asilimia 10,” alisema na kuongeza:
“Mimi ni mtu wa mabadiliko. Nina historia yangu... nimeshiriki
katika kuleta mabadiliko na nimeamini kutoka ndani ya moyo wangu kuwa
mabadiliko Tanzania ni lazima,” alisema.
Aidha,alisema amekuwa akifuatilia kampeni za vyama vya siasa
lakini ameshangazwa na kilichokuwa chama chake kuamua kupiga kampeni za
‘majitaka’, kwa kuruhusu watu kuwashambulia wengine wenye mitazamo
tofauti badala ya kueleza sera na kutoa ahadi kwa wananchi wanaotaka
wawachague.
“Nimekuwa nikifuatilia kampeni zinazoendelea nchini. Ukawa wametia
fora... wameonyesha ustaarabu, utulivu na heshima kwa nchi yetu,”
alisema.
“Kwa bahati mbaya, CCM ambayo ilikuwa ni chama changu, tangu
walipoanza kampeni wanafanya maajabu na vituko. Walianza kampeni za
matusi ya kustaajabisha. Licha ya CCM kuwa na sera nyingi, lakini
hawazungumzii sera. Wanazungumzia mtu,” alisema.
Aliongeza kuwa kuna watu wazima na wengine wamestaafu, lakini wote
wamechukuliwa na kupandishwa majukwaani kwa sababu moja tu ya
kumzungumzia mtu mmoja.
“Ukiona kila mtu anamzungumzia mtu mmoja, tena huyo huyo... jua kuwa mtu huyo atakuwa ni mzito sana. Siasa si uadui,” alisema.
Kuhusu marafiki zake waliobaki CCM, Kingunge alisema anawataka kutobabaika na badala yake wamchague rais wanayemtaka.
“Nimewaacha CCM kwa sababu siwezi kukubaliana na uongozi unaovunja
katiba za chama, taratibu za chama na unaowadhalilisha wagombea wa
urais. Kila mtu ana haki ya kumchagua rais anayemtaka,” alisema.
LOWASSA ATAKA KURA NYINGI
Wakati akizungumza jana, Lowassa alirudia tena kauli yake ya
kuwataka wananchi wajitokeze mapema siku ya kupiga kura na kumpa kura
nyingi za ndiyo ili kukabiliana vyema na vitendo vya wizi wa kura
vinavyoweza kufanywa na CCM.
Alisema jambo hilo ni muhimu kwani CCM ina historia ndefu ya wizi
wa kura na hivyo, njia pekee ya kuikabili hali hiyo ni kupiga kura
nyingi zaidi ili hata wakiiba, athari zake zisimnyime ushindi.
“Naomba kura nyingi kwa sababu hawa jamaa wana historia ya wizi wa kura. Pigeni kura nyingi,” alisema.
Akizungumzia uamuzi wa Kingunge, Lowassa alisema kuondoka CCM kwa
kada huyo mkongwe ni pigo kubwa na pia ni ishara nzuri ya kuwadia kwa
mabadiliko.
“Kingunge ni mzee lakini anaonekana kama kijana wa miaka 20... hili ni pigo kwa CCM,” alisema.
HUDUMA ZA AFYA
Akizungumzia huduma ya afya, Lowassa alisema iwapo atachaguliwa
kuwa rais atahakikisha kunakuwa na hospitali za wilaya katika kila
wilaya nchini.
Kadhalika, alisema akiingia madarakani, ataunda serikali makini itakayoshughulikia matatizo ya Watanzania.
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alisema tangu CCM iingie
madarakani hali ya uchumi imezidi kudidimia kutokana na ubadhilifu
unaofanywa na viongozi wa chama hicho na hivyo ni wakati mzuri sasa kwa
Watanzania kufanya mabadiliko kwa kumchagua Lowassa na wagombea wote wa
Ukawa.
Mwenyekiti wa NCCR - Mageuzi, James Mbatia, aliituhumu CCM kwa
kubebwa na serikali kupitia vitendo mbalimbali vyenye kuiwezesha kupata
fedha kwa njia haramu ili kuinufaisha.
HALI ILIVYOKUWA ARUSHA
Kabla ya kufanyika kwa mkutano huo jijini Arusha jana, maelfu ya
watu walijitokeza mapema asubuhi, kuanzia saa 5:00 asubuhi huku magari
na pikipiki zikipita huku na huko,
zikipambwa kwa bendera za Chadema.
Baadhi ya maduka yalifungwa na shughuli mbalimbali zilisimama.
Hata hivyo, amani ilitawala muda wote huku magari ya Jeshi la Polisi yakiranda randa huku na huko kulinda usalama.
Hadi kufikia saa 8:00 mchana, uwanja huo wa Sinon tayari ulikuwa
umefurika hadi watu wengine kuonekana wakikosa sehemu nzuri za kukaa.
0 comments:
Post a Comment