SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesaini mkataba wa miaka mitatu
na Kampuni ya Sahara Media wa haki ya kurusha mechi za Ligi Daraja la
Kwanza wenye thamani ya Sh milioni 450 jana.
Akizungumza kwenye hafla ya kusaini mkataba huo,Makamu Mwenyekiti wa
Sahara Media, Samwel Nyalla alisema kuwa Sahara Media kupitia Star TV
itakuwa ikionesha mechi za Ligi Daraja la Kwanza kuanzia msimu huu.
“Kila mwaka tutatoa milioni 150 kwa miaka mitatu kwa ajili ya haki ya
kurusha matangazo ya moja kwa moja ya ligi daraja la kwanza, ambayo
tayari imeshaanza kuchezwa”, alisema Nyalla.
Mkataba huo utazinufaisha timu zinazoshiriki ligi hiyo, ambapo kila
timu itapata milioni 15 kila msimu na fedha nyingine zitakazobaki
zitakuwa zikisaidia kuwalipa waamuzi pamoja gharama nyingine za michezo
ya ligi hiyo.
Nyalla alisema ligi hiyo itakuwa ikioneshwa kwenye king’amuzi cha Continental, ambapo malipo yake hayatazidi 10,000 kwa mwezi.
Pia alisema wanatarajia kuzindua chaneli mpya ambayo itafahamika kwa
jina la Star Sports Plus ambayo itakuwa inaonesha marudio ya mechi zote
za daraja la kwanza na ligi zingine ambayo itakuwa inaonekana kwenye
nchi zaidi ya 36 za Afrika.
Naye Rais wa Shirikisho la Soka, (TFF) Jamal Malinzi alimshukuru
Nyalla na uongozi wa Sahara Media kwa kukubali kuonesha ligi daraja la
kwanza kwani itasaidia kukuza soka kwa kuibua malalamiko ya waamuzi,
wachezaji na viongozi pia itasaidia kuwatangaza wachezaji nje.
“Ligi ikiwa inaoneshwa itasaidia kuuza wachezaji nje kwani mawakala
watakuwa wanafuatilia na kupunguza au kumaliza malalamiko juu ya
waamuzi”, alisema Malinzi.
Malinzi ameviomba vilabu vya FDL kutumia udhamini huo kama chachu ya
mafanikio na kufanya vizuri katika ligi hiyo itakayotoa timu tatu za
kupanda Ligi Kuu ya Vodacom (FDL) msimu ujao.
Aidha, Malinzi amewaomba wamiliki wa viwanja vinavyotumika kwa
michezo ya FDL kuviweka katika hali nzuri ya matunzo ili mechi
zinazochezwa katika viwanja hivyo ziweze kuwa nzuri kiufundi na
muonekano wa kwenye runinga.
Mkataba huo ni wa pili kusainiwa na TFF baada ya awali kusaini
mkataba na kampuni ya Star Times wenye thamani ya milioni 900. Jumla ya
thamani ya mikataba yote miwili (Star Times pamoja na Sahara Media) ya
udhamini wa ligi daraja la kwanza inafikia jumla ya Sh bilioni 1.35.
0 comments:
Post a Comment