MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward
Lowassa, ameionya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwamba kama haitakuwa
makini, inaweza kuvuruga uchaguzi mkuu.
Lowassa ambaye anaungwa mkono na vyama vinne vya siasa vinavyounda
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alitoa tahadhari hiyo alipokuwa
akihutubia mkutano wa kampeni katika viwanja vya Sabasaba, mjini Magu
jana.
Alitoa kauli hiyo kutokana na takwimu za wapigakura zilizotolewa na
Rais Jakaya Kikwete juzi, zikionyesha kutofautiana na takwimu za NEC.
Akizungumza katika kilele cha mbio za mwenge mjini Dodoma juzi, Rais
Kikwete alisema Watanzania waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la
Wapigakura kwa Tanzania Bara ni milioni 28 na Zanzibar ni zaidi ya
500,000.
Wakati Rais Kikwete akitoa kauli hiyo ambayo baadaye ilisahihishwa na
mwandishi wake msaidizi, Premi Kibanga, takwimu za NEC zinaonyesha
waliojiandikisha Tanzania Bara ni milioni 22.7 na Zanzibar ni 503,193.
Lowassa katika maelezo yake kwenye mkutano huo wa kampeni, alionyesha
kutoridhishwa na kauli ya Rais Kikwete kwa kile alichosema inatia shaka
kutokana na hali ya kisiasa ilivyo nchini.
“Jana (juzi) Rais Kikwete alitoa kauli kuhusu idadi ya wapigakura,
lakini baadaye kauli hiyo ikabadilishwa na kukanushwa kwa sababu ilikuwa
ikitofautiana na na ile ya NEC.
“Katika hili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina kazi kubwa, wasipoangalia
watavuruga, na uchaguzi ukivurugwa ni mwanzo wa matatizo katika nchi.
“Mimi sielewi, rais wa nchi anapewaje takwimu alafu baada ya saa
mbili zinakanushwa. Huyo anayempa rais wa nchi matakwimu ya namna hiyo
ni nani? Tulisema tume ni huru je, ni huru kwa hali hii ikiwa inangojea
taarifa ambazo zinatofautiana na za rais?
“Nataka kutoa tahadhari na kuwaomba wawe makini, wasituharibie
uchaguzi, wasituharibie nchi yetu, dhamana ya amani na utulivu juu ya
mambo haya iko juu yao, nawasihi sana wawe makini wasituharibie nchi,”
alisisitiza Lowassa.
Pamoja na suala hilo, Lowassa alizidi kuzungumzia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini na kusema hilo ni sawa na bomu.
“Mtu amesoma vizuri, anakaa nyumbani, kunakucha leo, kunakucha kesho, na kila siku hivyo hivyo, haiwezekani, atafanya lolote.
“Katika kukabiliana na hali hiyo, alisema Serikali yake itaboresha
kilimo na kukifanya kiwe cha kisasa ili kiweze kuajiri watu wengi,”
alisema.
Alisema sera ya kufuta kodi zote kwenye mazao ya chakula, inalenga kuhakikisha mkulima anafaidika na kilimo.
Njia ya pili aliyosema ataitumia kutoa ajira kwa Watanzania, ni
kuhakikisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linaongezewa uwezo mara tano
zaidi ya lilivyo sasa, ili pamoja na mambo mengine, litoe zaidi mafunzo
ya ufundi na stadi zitakazowawesha vijana kujiajiri.
MBOWE NA ELIMU YA KUPIGA KURA
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza
wa Ukawa, akizungumza na wananchi hao, alitoa elimu kwa wapigakura,
aliyosema inalenga kuokoa kura ambazo zinaweza kuharibika.
“Ukishapiga kura yako, ukunje karatasi wakati picha za wagombea
zikiwa zinaangalia nje, tofauti na ilivyozoeleka ambapo karatasi
hukunjwa picha na majina ya wagombea yakiwa ndani. Lengo la kukunja kura
picha za wagombea zikiwa nje ni kuepuka kura za maruhani ambazo
zitaharibika.
“Nawashauri pia wote mnaoweza kubeba kalamu zenu na kwenda nazo
vituoni, mwende nazo wala msiziamini zile za NEC. Mkishapiga kura kaeni
mita 200 ili kuzilinda.
“Wanasema tukipiga kura tukalale, hapa hakuna kulala, nyumbani
hatuendi, tutahesabu mita 200 tutapiga kambi mpaka matokeo yatangazwe,
uchaguzi ni maisha yetu na uchaguzi wa mwaka huu ni wa mabadiliko.
“Sisi tunasema hatutaki magari yasiyohusika kuingia vituoni, mkienda
kulala wataiba kura, polisi simamieni kura, msitake kuingiza taifa
kwenye machafuko, sisi tutasubiri matokeo, tutakesha hata kama yatatoka
kesho yake,” alisema Mbowe.
KINGUNGE
Kwa upande wa mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru,
pamoja na kuzungumzia masuala ya uchaguzi mkuu, alimzungumzia kada wa
CCM aliyekihama chama hicho, Balozi Juma Mwapachu.
Kwa mujibu wa Kingunge, kijana yeyote aliyekuzwa na Umoja wa Vijana
wa Tanu, hapaswi kubaki CCM kwa kuwa chama hicho kimepoteza mwelekeo.”
“Huyu kijana ana historia ndani ya CCM, kwani aliwahi kuwa kiongozi
wa Tanu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Huyo ni kati ya vijana wa
Tanu, vijana wa kweli wa Tanu Youth League ambao hawastahili kubaki
CCM,” alisema Kingunge.
0 comments:
Post a Comment