MWILI wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah
Kigoda, umezikwa katika Kata ya Chanika iliyopo Handeni mkoani Tanga.
Mazishi hayo yaliyofanyika jana yaliongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya wabunge wakati wa mazishi
hayo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema Serikali imepoteza mtu
mchapakazi, muadilifu na mwenye fikra za maendeleo ya mageuzi ya uchumi
wa nchi hii.
Alisema Dk. Kigoda alikuwa ni msomi aliyetumia taaluma yake katika
kushauri na kutetea masilahi mbalimbali ya taifa ili kujiletea maendeleo
endelevu.
Makinda alisema jambo ambalo hawatalisahau ni kusaidia kuleta mageuzi
ya kimfumo ndani ya Bunge hilo na kusaidia kuleta maendeleo makubwa.
“Tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi kutokana na michango mbalimbali
aliyoitoa na ushauri katika uendeshaji wa Bunge, hususani katika Kamati
ya Fedha na Uchumi aliyowahi kuiongoza,” alisema Makinda.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, akitoa salamu
za rambirambi kwa niaba ya Serikali, alisema Dk. Kigoda atakumbukwa kwa
kuwezesha kusimamia kwa vitendo mikakati ya kuendeleza biashara nchini.
Alisema aliweza kusimamia kwa ukaribu sera ya kuifanya nchi iweze
kujiendesha kupitia viwanda vikubwa, vya kati na vidogo katika kupiga
hatua za kimaendeleo kwa haraka.
Mwakilishi wa wabunge wa mkoani Tanga, Brigedia mstaafu, Hassan
Ngwilizi, alisema wamepoteza kiongozi aliyekuwa shujaa kwa mkoa huo na
taifa kwa ujumla.
“Marehemu alikuwa ni mwenyekiti wa wabunge wa mkoa huu, kila mara
alikuwa anatushauri na kutuasa ili kuhakikisha tunaleta maendeleo kwa
Serikali na wananchi wa mkoa huu,” alisema Ngwilizi.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya vyama vya upinzani, Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar,
Salum Mwalimu, alisema kuwa marehemu amewaachia jambo moja kuwa siasa si
ugomvi.
0 comments:
Post a Comment