TIMU ya soka ya Wilaya ya Magharibi imefanikiwa kusonga mbele katika
michuano ya Zanzibar CUP baada ya kuifunga Wilaya ya Kaskazini B mabao
3-2.
Mchezo huo ambao ni mwendelezo wa michuano hiyo ambayo inadhaminiwa
na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein ulichezwa juzi kwenye Uwanja wa
Amaan mjini hapa.
Katika Mchezo huo Wilaya ya Kaskazini B ndio waliotangulia kupata bao
dakika ya 19 tu kuanza kwa mchezo huo. Bao hilo ambalo liliwaamsha
Wilaya ya Magharibi lilifungwa na Mwinchuom Mbarouk na kusawazishwa
dakika mbili baadaye na Mkombozi Hakimu.
Magharibi baada ya kupata bao hilo walifanikiwa kuandika bao la pili
lililofungwa na Yussuf Juma dakika 25 wakati bao la tatu likiwekwa
kimiani na Mohammed Omar dakika ya 31.
Kwa upande wa Wilaya ya Kaskazini B bao lake la pili lilifungwa na
Suaka Mnyamis dakika ya 33. Kwa matokeo hayo Wilaya ya Magharibi
itashuka dimbani tena Oktoba 13 kucheza na timu ya Wilaya ya Kati katika
uwanja wa Amaan saa 10 jioni.
0 comments:
Post a Comment