KLABU ya Yanga jana ilisaini rasmi mkataba wa mwaka mmoja na nusu na
aliyekuwa Kocha Mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi kuwa msaidizi wa
Mholanzi Hans van der Pluijm.
Mwambusi juzi aliwaaga wachezaji, mashabiki na viongozi wa Mbeya City
tayari kutua Yanga kuchukua nafasi ya Charles Mkwasa aliyepewa mkataba
na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuifundisha Taifa Stars. TFF ilimpa
Mkwasa mkataba wa mwaka mmoja na nusu baada ya awali kuwa kocha wa muda
kufuatia kutimuliwa kwa aliyekuwa Kocha Mkuu Mholanzi, Mart Nooij.
Juzi Mwambusi alikutana na uongozi wa Mbeya City na kutumia fursa
hiyo kuaga rasmi huku uongozi ukimshukuru kwa yote mazuri aliyoifanyia
Mbeya City hadi kuwa moja ya timu tishio.
Mwambusi anatarajia kuanza kazi rasmi leo Jumatatu akiwa chini ya
Mholanzi, Hans van der Pluijm, ambaye akisaidiwa na Mkwasa waliiwezesha
timu hiyo kutwaa ubingwa msimu uliopita na kung’ang’ania kileleni msimu
huu baada ya kushinda mechi zote tano.
Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha alithibitisha jana kuwa Mwambusi
alisaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu na kusema kuwa waliachana na
mpango wa kumchukua kocha kutoka nje sababu Mwambusi analijua vizuri
soka la Tanzania.
Naye Katibu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema kuwa wanamtakia
kila la heri Mwambusi katika kazi yake hiyo ya kuifundisha Yanga.
Alisema kuwa klabu hiyo inachukua nafasi hiyo kumshukuru kocha huyo
kwa kazi yote nzuri aliyoifanya katika timu hiyo kwa miaka mitano akiwa
Mbeya City kwa kipindi hicho chote kwa mafanikio makubwa.
Mwambusi ni mmoja kati ya waanzilishi wa timu ya Mbeya City,hivyo
uongozi unatambua na kuthamini mchango wake mkubwa katika klabu hiyo
tangu kuanzishwa kwake.
Kwa sasa benchi la ufundi la Mbeya City FC litabaki kuwa chini ya
kocha msaidizi Meja Abdul Mingange (Rtd.) mpaka itakapotolewa taarifa
nyingine.
Mwambusi amewaachia simanzi viongozi wa Mbeya City, timu ambayo
aliipandisha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2013- 2014 na
kuwa tishio nchini ndani ya muda mfupi.
0 comments:
Post a Comment