TIMU ya taifa ya Tanzania Taifa Stars pamoja na kupokea kichapo cha
bao 1-0 kutoka kwa Malawi `The Flames’ imesonga mbele katika
kinyang’anyiro cha kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika
Urusi 2018.
Katika mchezo huo uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Kamuzu Banda
jijini Blantyre, Malawi, na wenyeji walipata bao hilo pekee katika
mchezo huo na kuifanya Taifa Stars kupenya kwa ushindi wa jumla ya mabao
2-1, baada ya kushinda 2-0 nyumbani.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi wa Angola, Martins de
Carlvalho aliyesaidiwa na Gadzikwa Bongani wa Zimbabwe na Valdmiro
Ntyamba wa Angola, hadi mapumziko wenyeji walikuwa mbele kwa bao hilo
1-0.
Taifa Stars ilicheza na Malawi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam Jumatano iliyopita huku mabao yake yakifungwa na wachezaji
wanaocheza soka TP Mazembe ya Congo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Taifa Stars sasa itakutana na Algeria inayoshika nafasi ya kwanza kwa
ubora barani Afrika huku ikishika nafasi ya 19 kwa ubora duniani kwa
mujibu wa viwango vilivyotolewa mwezi huu na Shirikisho la Kimataifa la
Soka (Fifa).
Malawi inashika nafasi ya 101 wakati Tanzania iko katika nafasi ya
136 kwa ubora huo wa soka. Katika mchezo huo wa jana, Malawi waliandika
bao la kuongoza katika dakika ya 41 lililofungwa na Chimanga Kayira
baada ya kupiga shuti la kiufundi lililomgonga Kelvin Yondani mgongoni
na kujaa wavuni.
Mchezaji wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa nchini Congo katika
timu ya TP Mazembe, Mbwana Samatta alipofanikiwa kufanya shambulizi
katika dakika ya kwanza ya mchezo, alipiga shuti lakini liliokolewa na
kipa wa Malawi.
Wenyeji walijibu mapigo katika dakika ya tatu na kulisakama lango la
Taifa Stars walipofanya shambulizi la maana na beki Nadir Haroub
alizubaa na kuwafanya Malawi kupata upenyo na kupiga shuti, lakini kipa
Mustapha Bertez alifanya kazi ya ziada kuokoa mchomo huo na kuwa kona,
ambayo haikuzaa matunda.
Katika dakika ya 14, Ulimwengu aliangushwa katika eneo la hatari na
kuumia, lakini mwamuzi alipeta. Dk ya 10 Kayira alipiga shuti kali,
hatari, lakini Barthez aliokoa na kugonga mwamba na kurudi uwanjani.
Malawi katika dakika ya 32 walifanya shambulizi la nguvu, kwa krosi safi
ya Chiyasa, lakini Barthez kwa mara nyingine alifanya kazi ya ziada na
kuokoa mpira huo.
Tanzania ilifanya kazi nzuri katika dakika ya 34 baada ya Thomas
Ulimwengu kubaki yeye na lango mbele ya makipa, lakini alishindwa
kulenga lango na kuikosesha Taifa Stars bao la kuongoza.
Hiki ni kipigo cha kwanza kwa kocha Charles Mkwasa katika mechi za
mashindano, ambapo akiwa kocha wa muda Stars ilitoka sare ya kufungana
1-1 na Uganda katika mchezo wa Chan na baadaye kutoka suluhu na Nigeria.
Huku baada ya kupewa mkataba wa mwaka mmoja na nusu, timu hiyo
ilishinda 2-0 katika mchezo wa awali dhidi ya Malawi jijini Dar es
Salaam. Katika historia ya Tanzania, Taifa Stars haijawahi kufuzu kwa
fainali za Kombe la Dunia.
0 comments:
Post a Comment