Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amekanusha uzushi
kuwa amesambaza taarifa kwenye mitandao ya kijamii yenye kichwa cha
habari ‘Mengi ajitoa rasmi kwa Lowassa’ na kusisitiza kwamba taarifa
hizo ni za uongo, upotoshaji na uchochezi.
Dk. Mengi alikanusha uzushi huo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
“Nimeomba tukutane (waandishi wa habari) leo (jana) kwa jambo moja
tu. Kuwafahamisha kwamba taarifa inayoenezwa kupitia mitandao ya kijamii
yenye kichwa cha habari kinachosema; ‘Mengi ajitoa rasmi kwa Lowassa’
na eti nimesema: Kama jamaa (Ukawa) watashinda nafasi ya urais, basi ni
baada ya miaka 10 siyo hivi sasa, taarifa hiyo ni ya uongo, upotoshaji
na uchochezi,” alisema.
Ukawa ni Umoja wa Katiba ya Wananchi unaoundwa na vyama vinne vya
Chadema, Cuf, NCCR- Mageuzi na NLD, ambavyo kwa pamoja vimemsimamisha,
Edward Lowassa, kuwania nafasi ya urais kupitia Chadema katika Uchaguzi
Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Dk. Mengi alisema taarifa za aina hiyo zisipokemewa na kuchukuliwa hatua za haraka zinaweza kuathiri amani ya taifa.
“Ni matarajio yangu kwamba vyombo husika vitachukua hatua zinazostahili kwa haraka iwezekanavyo,” alisema, Dk. Mengi.
Dk. Mengi mara kwa mara amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuzingatia
amani na kuepuka uchochezi na mambo yanayoweza kuliingiza taifa kwenye
machafuko katika kipindi hiki cha kabla, wakati na baada ya Uchaguzi
Mkuu.
0 comments:
Post a Comment