RAIS Jakaya Kikwete ametaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
kutafuta njia za dharura kukabili hali ya umeme nchini, ambayo ni mbaya.
Alitaka Tanesco iongeze kasi kufanya majadiliano na kampuni
iliyojitokeza kuleta umeme, lakini kwa kuhakikisha wanafuata sheria na
taratibu, isije yakatokea ya miaka ya nyuma, yaliyosababisha kidonda
mpaka leo. Alisema hayo juzi, alipozindua rasmi miundombinu ya kuchakata
na kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi jijini Dar es
Salaam.
Kikwete alisema hali ya umeme nchini ni mbaya kutokana na ukame
uliojitokeza, kama wa mwaka 2006. Hata hivyo, alisema ingawa hali hiyo
inaonesha kuzunguka kila baada ya miaka 10, ni bahati ulifanyika uamuzi
mapema wa ujenzi wa bomba la gesi, vinginevyo hali ingekuwa mbaya zaidi.
Alisema juzi Tanesco waliingiza megawati 70 za umeme kutoka mtambo wa
Kinyerezi na baada ya wiki moja, wataingiza megawati 80 kwa kutumia
gesi asilia. Lakini, alisema megawati zilizopotea kwa umeme wa maji ni
nyingi kuliko zinazoingia, hivyo tatizo kuendelea kuwapo.
“Nimewaagiza Tanesco kuwa hali hiyo sasa siyo ya kawaida, lazima
kufanya uamuzi ambao siyo wa kawaida kwa kutafuta ufumbuzi, lakini
wazingatie sheria na taratibu ili kupata mbadala na isilete tatizo kama
awali,” alisema. Rais Kikwete alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco,
kuhakikisha umeme unapatikana ili kuondolea shaka wananchi.
“Ongezeni kasi ya mazungumzo na wanaotaka kutupatia umeme kwa
kufikisha megawati 970 huku mahitaji yakiwa 940 pamoja na kuwa na umeme
wa dharura, ili nchi isiingie kwenye matatizo ya mgao,”alisisitiza.
Alisema gharama ya ujenzi wa miundombinu hiyo ni kubwa, lakini
ilimlazimu kukopa kutokana na umuhimu wake katika kukabiliana na tatizo
la umeme nchini.
Akizungumzia ukame katika mabwawa ya kuzalisha umeme, Kikwete alisema
Kidatu yenye uwezo wa kuzalisha megawati 240, hivi sasa inazalisha
megawati 27.
Mabwawa mengine ni Kihansi ambayo inatakiwa izalishe megawati 180,
lakini zinazalishwa megawati 45, na Pangani megawati 68 na sasa
zinazalishwa 25. Kwa upande wa bwala la Mtera, uzalishaji umefungwa
baada ya kina cha maji kufika 687 na hivyo mtambo kuingiza tope.
Tanesco yajipanga
Akizungumzia ushauri wa Rais Kikwete, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco,
Felchesmi Mramba alisema wameanza mazungumzo ya awali na kampuni ya
kuzalisha umeme kwa wingi na haraka na muda si mrefu watatoa taarifa
walipofikia.
Huduma za jamii
Akizungumzia huduma za jamii kwa vijiji vinavyopitiwa na miundombinu
na uchimbaji gesi, Rais Kikwete alilitaka Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC) kuwachimbia visima wanavijiji, waache
wanaolalamika gesi kuchukuliwa wakati wao wakibaki na shida ya maji.
“Msipofanya hivyo mtakuwa na mgogoro usioisha,” alisema. Alisisitiza,
“Huu ni wajibu kwa jamii inayowazunguka haina mjadala, tafuteni
ufumbuzi ili muishi vizuri; pia wasaidieni katika zahanati na shule
kwani hali ni mbaya.”
0 comments:
Post a Comment