Mahujaji wengine wawili
kutoka Tanzania ambao walikuwa hawaonekani tokea ajali ya kukanyagana kwa
mahujaji ilipotokea Makkah nchini Saudi Arabia tarehe 24 Septemba 2015
wametambuliwa kuwa, ni miongoni mwa mahujaji waliofariki dunia. Kutambuliwa kwa mahujaji hao kunafanya
idadi ya mahujaji wa Tanzania waliopoteza maisha katika ajali hiyo kufikia
ishirini na saba (27). Majina kamili ya mahujaji hao ni Bw. Juma Yussuf Bakula
na Bw. Ahmad Awadh Namongo kutoka Kikundi cha Ahlu Dawaa.
Hadi sasa mahujaji
kumi na tatu (13) kutoka Tanzania bado hawajulikani walipo na jitihada za
kuwatafuta bado zinaendelea.
Kwa upande wa
mahujaji wanne ambao walikuwa wanapatiwa matibabu kutokana na kuugua au
kujeruhiwa, mmoja wao ni Bw. Mustafa Ali Mchina ambaye alikuwa amelezwa katika
chumba cha wagonjwa mahututi katika mji wa Maddinah alifariki dunia tarehe 17
Oktoba 2015 na kuzikwa Maddinah siku hiyo hiyo. Bi. Mahjabin Taslim Khan ambaye
alijeruhiwa katika ajali hiyo na kusababisha kukatwa mguu wake amepata nafuu na
alirejea nchini tarehe 20 Oktoba 2015. Mwingine ni Bi. Hidaya Mchomvu ambaye
alijeruhiwa pia bado yupo hospitali akiendelea kupatiwa matibabu. Hujaji wanne
ni Bw. Ahmed Abdallah Jusab ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo alifanyiwa
upasuaji wa kumuwekea kifaa cha kuongeza mapigo ya moyo tarehe 19 Oktoba 2015
na alitarajiwa kurejea nchini tarehe 21 Oktoba 2015.
Serikali ya Saudi
Arabia inaendelea kutoa taarifa zaidi za kuwatambua mahujaji waliofariki dunia
au kujeruhiwa katika ajali hiyo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu wahanga wa ajali hiyo kadri
itakapokuwa inazipokea.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
22 Oktoba, 2015
0 comments:
Post a Comment