Rais Jakaya Kikwete, jana aliongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es
Salaam kuuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Democratic Party (DP),
Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye jeneza lake lilipambwa kwa Bendera
ya Tanganyika kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, jana.
Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine waliohudhuria tukio hilo
kabla mwili wa marehemu haujasafirishwa kwenda kwao mkoani Njombe ni
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Ghalib
Bilal na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Maalim Self Shariff Hamad na viongozi wa vyama vya siasa na dini.
Akizungumza kabla ya kuagwa kwa marehemu, Dk. Bilal alisema Mtikila
atakumbukwa kwa ujasiri wake wa kusimamia kile alichokuwa akikiamini na
pia mchango wake katika siasa nchini.
Kadhalika, Dk. Bilal alisema kupitia harakati zake mbalimbali,
Mtikila amesaidia kuudhihirishia ulimwengu ni kwa namna gani Tanzania
inatoa uhuru wa kujieleza kwa wananchi wake.
“Hata mimi nilikuwa napata wakati mzuri wa kuzungumza na marehemu
Mtikila. Na wakati ule alikuwa akitoa mchango mkubwa sana kwa vyuo
vikuu, hata pale tulipokuwa tukikwazana katika harakati zake hizo, bado
tulikuwa tunapata muda wa kuzungumza na kumaliza tofauti zetu. Hivyo
tunataka Tanzania inayoruhusu mawazo tofauti,” alisema Dk. Bilal.
Maalim Self alisema Mtikila alikuwa muwazi na ambaye hakuwahi kumuogopa mtu, na mara zote alipenda kusimamia kile alichokiamini.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema Mtikila
atakumbukwa kwa mchango wake katika masuala ya sheria kwa vyama hivyo,
akiongeza kuwa ataenziwa kwa utii wa sheria pale alipopigania kile
alichokiamini, hasa kwa kutumia vyombo vya sheria kudai haki pasipo
kufanya maandamano.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Kuga Mziray, alisema
bado mchango wa Mtikilia ulikuwa unahitajika, hasa katika kipindi hiki
cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Makamu Mwenyekiti wa DP Zanzibar, Peter Mapwila, alisema wamepata
pigo kubwa kumpoteza kiongozi wao na kwamba katika kumuenzi, wamepanga
kuendeleza mambo ya msingi aliyokuwa akisimamia hasa uwapo wa
Tanganyika.
Dada wa Marehemu, Maria Mtikila, pamoja na kushukuru kwa faraja
ambayo wamepata kutoka kwa watu mbalimbali tangu kuondokewa na mpendwa
wao, pia alisema Mtikila kwao alikuwa chachu ya familia, aliyetegemewa
kwa mambo mbalimbali na kwamba wanamfananisha na nuru ambayo sasa
imezimika.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufunuo Tanzania, Paul Bendera, alisema ni
vema Watanzania wakajitambua na kuwa makini katika kuheshimu maisha ya
mtu, kudumisha upendo, amani na uhuru wa maisha ya kila mtu.
Mchungaji Mtikila, pamoja na kujishughulisha na mambo mbalimbali,
pia alianza kujikita katika masuala ya siasa miaka ya 1990 ikiwamo
kuanzisha chama chake cha DP.
Akisoma wasifu wa marehemu, Victor Manyai, alisema Mtikila
alizaliwa Juni 7 mwaka 1950 katika Kijiji cha Milo, wilayani Ludewa,
mkoani Njombe.
Alifariki kwa ajali ya gari Oktoba 4, mwaka huu katika Kijiji cha
Msolwa, mkoani Pwani wakati akitokea mkoani Njombe kwenye kampeni za
uchaguzi za wagombea udiwani na ubunge wa chama chake katika Jimbo la
Njombe Kusini.
0 comments:
Post a Comment