MGOMBEA ubunge wa Chama cha ACT- Wazalendo Jimbo la Bariadi Magharibi,
Masunga Joseph Nghezo ametekwa na watu wasiojulikana akiwa kwenye
harakati za kufanya mikutano ya hadhara katika jimbo hilo.
Mbali na kutekwa pia simu yake aliyokuwa akiitumia ndiyo inatumika
kutuma ujumbe wa vitisho kwenda kwa mzazi wa mgombea huyo ikimtaka
amkanye mwanae kuachana na siasa vinginevyo familia nzima itadhurika.
Taarifa ya chama hicho iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisa Habari
wake, Dar es Salaam jana Abdallah Khamis ilisema kuwa siku ya Jumatatu,
Nghezo alikuwa akijiandaa kwenda katika mkutano wa hadhara Kijiji cha
Baneni.
Alisema kabla ya kutoweka kwake, Nghezo alienda kumtafuta dereva
mwingine wa kumuendesha baada ya yule wa siku zote kwenda msibani na
aliporudi na dereva mwingine aliliacha gari likiwa katika maandalizi ya
kufungwa vipaza sauti.
Aliongeza baada ya dereva na viongozi wengine wa chama hicho kumaliza
kazi ya kufunga vipaza sauti walianza kumtafuta mgombea wao bila
mafanikio huku simu yake ikiwa haipatikani hadi jana (juzi) mzee wake
alipopokea ujumbe mfupi wa simu kupitia simu ya mwanae ikimtaka kumkanya
mwanae aachane na siasa za Bariadi.
Khamis alieleza kuwa baada ya ujumbe huo siku ya juzi Mzee Nghezo,
alitumiwa ujumbe mwingine wa simu ukimueleza kuwa wanampa muda wa saa
sita kutekeleza masharti yao vinginevyo watamdhuru kijana wake na kisha
kuitafuta familia nzima.
“Siku ya Jumanne zilianza kuingia meseji ya vitisho kwenda kwa mzazi wa
mgombea wa ACT-Wazalendo zikimtaka mzazi huyo amkanye mwanae kwa kuwa
amekuwa kikwazo kwa watu wengine kulipata jimbo hilo,” alisema.
Alisema meseji nyingine zikatumwa kwa mzazi wa mgombea juzi jioni
zikieleza kuwa wametoa muda wa saa sita kwa masuala yao kutekelezwa
vinginevyo watafanya wanachokijua.
Pia, alisema kutekwa kwa mgombea wao katika Jimbo la Bariadi Magharibi
ni muendelezo wa hujuma dhidi ya chama chao kwa kuwa katika siku za hivi
karibuni wagombea wa majimbo ya Chilonwa mkoani Dodoma na Bariadi
Mashariki (Itilima), walitishwa na baadhi yao kuharibiwa magari na watu
wasio julikana
“Juzi tulitoa taarifa ya mgombea wa Itilima, Issac Nyasilu kuharibiwa
gari lake na hii ni baada ya kukataa kujitoa katika kinyang’anyiro cha
ubunge wa Itilima, huko Chilonwa mgombea wetu Eva Mpagama anatishwa kila
siku sasa wameamua kumteka kabisa huyu wa Bariadi Magharibi,” alisema
Khamis.
Aliliomba jeshi la Polisi kuingilia kati uharamia huo na kuwafikisha
katika vyombo vya sheria wahusika ili iwe fundisho kwa watu wasiolitakia
mema Taifa la Tanzania.
Kwa vyama vya siasa, Khamis alisema ni vema wakajikita kujenga hoja
zitakazowafanya kukubalika mbele ya jamii badala ya kutumia nguvu na
vitisho kutafuta nafasi ya kuwaongoza wananchi.
0 comments:
Post a Comment