TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema waliopoteza vitambulisho vya
kupigia kura wataweza kupiga kura endapo watakuwa na taarifa ya polisi
na majina yao kuwamo katika daftari la mpiga kura.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Kamishna wa NEC, Mary
Stelalongwe alipotoa ufafanuzi kuhusu watu wanaozunguka mitaani
kuandika namba za vitambulisho vya wapiga kura.
ameonya kuwa kufanya hivyo ni kosa ingawa alisema NEC haina taarifa rasmi ya matukio hayo.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema tume
imepeleka taa katika vituo vyote vya kupigia kura kuepuka kura
kuhamishwa na kuhesabiwa sehemu nyingine.
“Tunasema kura zitahesabiwa katika kituo husika lakini inapotokea
hiyo sehemu haina taa inabidi kura hizo zihamishiwe katika kituo chenye
taa ambako zitasindikizwa na mawakala na zitatenganishwa na za kituo
hicho,”alisema Lubuva.
Alisema ili kuepuka hali hiyo Tume imesambaza taa katika vituo vyote vya kupigia kura ambavyo ni 72,000 nchi nzima.
Akizungumzia mchango wa vyombo vya habari katika uchaguzi huu,
aliviomba viisaidie tume kutoa taarifa sahihi uchaguzi uwe wa amani.
“Vyombo vya habari vikiwa mstari wa mbele na kufanya kazi yake kwa
umakini bila kupotosha vitaisaidia Tume iendeshe uchaguzi katika hali ya
amani na utulivu,” alisema Lubuva.
Alisema vyombo vya habari havitaruhusiwa kutangaza mshindi wa
uchaguzi kabla ya kutangazwa na mamlaka husika lakini wanaruhusiwa
kuripoti matokeo ya vituoni kama yalivyo.
Mwenyekiti wa Chama cha wamiliki wa vyombo vya Habari (MOAT), Dk.
Reginald Mengi, aliilaumu tume kushindwa kuvichukulia hatua kali vyama
vinavyokiuka maadili ya uchaguzi.
“Tumeshuhudia watu wanatumia lugha za chuki, kutukanana na
kukashifiana lakini tume imekuwa ikitoa kauli za jumlajumla badala ya
kushughulika na yule aliyekosea,” alisema Dk. Mengi
Akijibu hoja hiyo, Lubuva alisema Tume imekuwa ikipokea malalamiko mengi na imekuwa ikivionya vyama huzika.
Alisema hatua zaidi hutakiwa kuchukuliwa na kamati ya maadili ambayo
inaundwa na wagombea wenyewe kitu kinachosababisha kushindwa kukaa mara
kwa mara.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Emmanuel Kawishe, alivikumbusha vyombo
vya habari kupeleka majina ya waandishi watakaoripoti uchaguzi kwa vile
zimeongezwa siku za kuwasilisha majina hadi Oktoba 5 badala ya Septemba
30 (jana)
“Hadi sasa tumepokea majina 311 na tumefanyia kazi majina 151 na
mengine na mengine 160 yanaendelea kufanyiwa kazi na kwa upande wa
vyombo vya nje tumepokea majina 11, matano tumeyafanyia kazi na sita
yanaendelea kufanyiwa kazi,” alisema Kawishe.
0 comments:
Post a Comment