Image
Image

NCCR - Wanasa mbinu chafu za kuiua UKAWA*Mbatia naye asukiwa mkakati wa kummaliza.

CHAMA cha NCCR Mageuzi kimetibua njama za kuuhujumu na kuufarakanisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) zilizolenga pia kusababisha mauaji kwa Mwenyekiti wake, James Mbatia.
Akizungumza   na waandishi wa habari   Dar es Salaam,Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia aliyefuatana  na viongozi wa juu wa chama hicho, alisema mkakati huo uliwahusisha makamishna wa chama hicho waliohudhuria pia mkutano huo, na uliratibiwa na Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Leticia Mosore.
Huku akionyesha vielezo vya picha na video, Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alidai  Mosore ametenda makosa ya jinai yakiwamo ya kupanga njama za kudhuru na mauaji hivyo   ushahidi huo unapelekwa polisi kwa hatua zaidi.
Alidai  Mosore alianza hujuma hizo Septemba 17 mwaka huu kwa kuzungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Land Mark   Dar es Salaam ambako alitoa waraka uliolaumu hatua ya chama hicho kujiunga na Ukawa.
“Cha kusikitisha ni   baadhi ya viongozi wa juu wa chama wanapokwenda kinyume na Katiba na sheria za chama. Tarehe 17 Septemba mwaka huu, Mama Leticia Mosore alizungumza na waandishi wa habari na kumlalamikia mwenyekiti kuwa anadhoofisha chama na amekuwa msemaji wa Chadema,” alisema Mbatia.
Hata hivyo, Mbatia alimtetea Katibu mkuu wa chama hicho aliyekuwapo pia kwenye mkutano huo,   akisema hakuzungumzia mambo ya chama bali migongano tu ya Ukawa.
“Katibu Mkuu, Nyambabe Mosena alikuwapo ila hakuzungumzia mambo ya chama bali migongano ya Ukawa ambayo tunakubaliana,” alisema.
Alisema  Mosore amekiuka katiba ya chama hicho na kwamba na amesimamishwa uongozi huku hatua nyingine zikifuata.
“Baada ya kikao chake tulimwita katika kikao nilichokiongoza mimi mwenyewe na alijitetea na mengine akakiri. Kikao kile kwa niaba ya Halmashauri Kuu kilimsismamisha uongozi,” alisema.
Aliendelea kumtuhumu Mosore kuwa alikula njama kwa kuwatumia fedha makamishina wa chama hicho kwa ajili ya kupanga mpango wa kumdhuru na kumfarakanisha na Ukawa.
“Alikuwa akituma fedha kwa makamishina hawa na alishirikiana na CCM, ushahidi upo. Kwa mujibu wa Katiba yetu, ukihujumu chama kwenye uchaguzi unafukuzwa uanachama.
“Septemba 17 nilipokea ujumbe wa kutishiwa maisha na kulikuwa na taarifa za wanachama wa chama chetu kuvalishwa sare ili wanivamie na kunidhuru,” alidai  Mbatia.
Alisema kutokana na tishio hilo, Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini wa chama hicho, Mohamed Tibanyendera alitoa taarifa na kufikisha taarifa   Polisi.
Alisema katika mkakati huo waliwatumia makamishina wanne wa chama hicho ambao ni Peterson Mshenyera kutoka Kagera, Rajab Mawaya kutoka Mkoa wa Pwani, Ame Mshindani kutoka Kaskazini Unguja na Rajab Amran kutoka Mwanza kwa kuwalipia fedha za kujikimu (Sh 60,000 kila siku na tiketi za ndege).
Licha ya fedha hizo, alisema makamishina hao walilipwa Sh 400,000 jana na waliahidiwa kupewa Sh milioni 10 kama kiinua mgongo chao na walikuwa wakifanya vikao eneo la Segerea   Dar es Salaam kwa kada wa CCM aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya (jina linahifadhiwa) tangu Septemba 22.
“Leo (jana) walitakiwa waende Hoteli ya Peacock kusoma waraka walioandaliwa. Lakini kwa kuwa tulikuwa tunawasiliana tangu awali, tuliwachukua na kuwapeleka sehemu nyingine na simu zao zikabadilishwa. Ndiyo maana mlisikia kuwapo  mkutano wa habari pale,” alisema Mbatia.
Akizungumzia njama hizo, kamishna wa chama hicho, Peterson Mshenyera alisema   alihusishwa tangu Septemba 19.
“Nilihusishwa kwenye mkakati huo siku mbili baada ya kuzungumza na waandishi wa habari. Ninavyo vielelezo kwenye simu yangu. Awali nilisita lakini niliwasiliana na Mwenyekiti na akaniimarishia ulinzi,” alisema Mshenyera na kuongeza:
“Waliongeza makamishna wengine bila kujua kuwa ndiyo wanaharibu. Leo tumelipwa Sh 400,000 na tuliahidiwa Sh milioni 10.”
Huku akisitiza kutomtaja   jina, Mshenyera alisema kuna kiongozi wa CCM ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya mojawapo ya chama hicho aliyekuwa akiratibu njama hizo.
“Siwezi kumtaja kiongozi huyo kwa sababu hawa watu wana hela nyingi, nahofia usalama wangu. Huu waraka una maneno ya kumtukana Lowassa (Edward- mgombea urais wa Ukawa), Sumaye (Frederick- Waziri Mkuu mstaafu) na Ukawa na unavitaka vyama vya CUF na NLD kutopigia kura Ukawa,” alisema.
Alisema baada ya kusoma waraka huo walipanga kusafiri nchi nzima kuutangaza na mpango wa pili ulikuwa ni kuivuruga halmashauri kuu ya chama hicho na mwisho kuuvuruga mkutano mkuu.
“Tumesema hatuwezi kumtukana baba yetu, hatuwezi kukiharibu chama chetu na kutukana Ukawa,” alisema.
Alipotafutwa kwa njia ya simu, Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Leticia Mosore alisema hana taarifa za kusimamishwa uongozi wala njama hizo.
“Hizo taarifa siyo za kweli, kwanza mimi naumwa niko nyumbani. Hapa nilipo nasikia baridi   nataka kwenda hospitali,” alisema Mosore.
Alikiri kuitwa kwenye kikao cha viongozi wa juu wa chama hicho, Septemba 18, lakini akasema walijadili masuala ya chama.
“Ni kweli tulikuwa na kikao na tulijadili mambo ya chama. Hayo mengine mimi sijui, niko nyumbani naumwa. Wewe ni mwandishi wa pili kunipigia simu kuuliza mambo hayo,” alisema Mosore.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment