TAASISI nne zinazojihusisha na masuala ya afya ya binadamu,zimekubaliana kwa pamoja kuunga mkono mabadiliko katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 25 mwaka huu.
Taasisi hizo ni Jumuia ya Madaktari Tanzania (MAT), Chama cha Wauguzi
Tanzania (TANNA) Jumuia ya Wafamasia Tanzania (PST) pamoja na Jumuiya
ya Madaktari Wasaidizi Tanzania (AMEPTA).
Viongozi wa taasisi hizo walitoa tamko hilo la pamoja katika Ukumbi
wa Hoteli ya Mtakatifu Theresa,mjini Bukoba mkoani Kagera jana
wakisema wanaunga mkono mabadiliko ya siasa kuelekea uchaguzi mkuu
ikizingatiwa sekta ya afya inakabaliliwa na changamoto nyingi, hivyo
inahitaji mabadiliko ya siasa kupata muafaka wa afya ya Watanzania.
Akisoma tamko hilo kwa kwa niaba ya wenzake, Rais wa TANNA, Paulo
Magesa, alisema wao kama vyama vya kutetea maslahi ya watumishi wa sekta
ya afya wanaunga mkono mabadiliko yatakayotokea nchini ingawa
hawakuweka wazi mabadiliko hayo ni ya chama kipi cha siasa.
Tamko hilo limebeba kauli mbiu isemayo, “Afya bora kwa wote inawezekana Tanzania, tuamue Oktoba 25”.
Katika tamko hilo, taasisi hizo zimeainisha changamoto mbalimbali
zinazoikabili sekta ya afya ikiwa ni pamoja na ukosefu wa dawa, vifaa
tiba na vifaa vya uchunguzi vya kutosha zikisema tatizo hilo
linasababishwa na bajeti finyu ya sekta ya afya hususan inayoelekezwa
katika upatikanaji wa dawa.
Pia ukosefu wa viwanda vikubwa vya kuzalisha dawa za kutosha zenye
ubora stahiki vinavyomilikiwa na serikali na ucheleweshwaji wa malipo
kwa ajili ya dawa katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kutoka serikalini na
hivyo kuifanya MSD kushindwa kuagiza dawa za kutosha nje ya nchi.
Changamoto nyingine ni kuwapo msambazaji mmoja wa dawa yaani MSD
pekee kwa vituo vyote nchini huku akiwa hajajengewa uwezo wa kutosha na
hivyo wakati mwingine kusababisha uchelewaji wa dawa na vifaa tiba
katika vituo vya afya.
Akisoma tamko hilo, Magesa alisema hadi kufikia mwaka 2014 uhaba wa
wafanyakazi katika sekta ya afya ulikuwa ni asilimia 56, ambayo ni nusu
ya wafanyakazi wanaohitajika na hivyo kusababisha watumishi wachache
waliopo kufanya kazi kubwa na hata wakati mwingine zilizo nje ya wigo wa
majukumu yao.
Magesa alisema wamechukua hatua hiyo madhubuti wakati taifa likiwa
katika maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu ifikapo Oktoba 25, mwaka huu
huku akisisitiza kuwa wanatambua mstakabali na msingi wa mabadiliko ya
kweli katika sekta ya afya na hata sekta nyingine za maendeleo zimo
mikononi mwa wanasiasa wanaotarajiwa kuchaguliwa, kuanzia madiwani,
wabunge na raisi.
Alisema mfano mwaka 2014 pekee, daktari mmoja Tanzania alihudumia
wastani wa watu 20,000 tofauti na wastani wa watu 5,000 unaotakiwa kwa
mujibu wa kanuni za kitaalamu uliowekwa na Shirika la Afya Duniani
(WHO).
Alisema uhaba huo unachangiwa kwa kiasi kikubwa kutokuwapo vyuo
vya kutosha kwa ajili ya kutoa mafunzo katika kada za afya ambapo mwaka
2014 vyuo vyote vilitoa wastani wa wahitimu 9,000.
“Kwa malengo ya kuwa na zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya
kila kata na hospitali kwa kila wilaya nchi nzima tulipaswa kuwa na
wastani wa wahitimu 20,000 kwa mwaka kuanzia mwaka 2008 huku pia
serikali ikishindwa kuajiri wahitimu wote wanaomaliza katika vyuo
vichache vilivyopo.
“Kwa mfano, kwa kada ya udaktari pekee katika wahitimu 700, wahitimu
chini ya 300 huajiriwa kila mwaka huku wahitimu 400 waliosoma kwa fedha
za serikali wakiwa hawaajiriwi serikalini na hivyo kuamua kufanya kazi
nje ya sekta ya afya.
“Hadi mwaka huu wapo wagonjwa wanaolala chini katika hospitali zetu,
wapo wanaolala zaidi ya wawili kitanda kimoja na wapo ambao inabidi
kuruhusiwa kabla ya kupona vizuri kutoa nafasi kwa wenye hali mbaya
zaidi. Hii huwavunja moyo watoa huduma na hata wakati mwingine kushindwa
kutoa huduma inayostahili kwa wananchi.
“Zipo sera za huduma bure kwa makundi maalumu, hata hivyo mara
nyingine utekelezaji wake umesongwa na uhaba wa dawa na vifaa tiba hata
kuleta migogoro kati ya watoa huduma na wahudumiwa.
“Kwa nini tunachukua hatua hii wakati huu kuelekea Uchaguzi Mkuu
ifikapo Tarehe 25 Oktoba, jibu ni kwamba tunatambua mustakabali na
msingi wa mabadiliko ya kweli katika sekta ya afya na hata sekta
nyingine za umma umo mikononi mwa wanasiasa tunaokwenda kuwachagua
kuanzia madiwani, wabunge na rais.
“Hivyo tungependa wahudumu au wataalam wa afya na wananchi wote
watambue wanapoamua kuacha kupiga kura au wanapopiga kura basi wanaamua
mustakabali wa afya yao katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Hivyo lengo letu kuu ni kuwaelimisha wadau wa afya wote nchini
kwamba tusifanye makosa, tuamue afya yetu sasa, tuchague kwa makini,
tuchague mabadiliko ya kweli,” alisema rais huyo wa TANNA.
Naye mgeni rasmi katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John
Mongella alisema baadhi ya changomoto zilizoibuliwa na wataalamu hao wa
sekta ya tiba zitatafutiwa ufumbuzi.
“Kweli kama serikali tuna wajibu wa kushughulikia changamoto katika
sekta ya afya, sekta hii ni nyeti tunawajibika kutimiza wajibu, baadhi
ya changamoto naamini zinawezekana kutatuliwa kama tutajenga utaratibu
wa kukaa pamoja na changamoto nyingine ni ubunifu tu ambazo hazihitaji
mjadala wa taifa” alisema Mongella.
0 comments:
Post a Comment