HUKUMU ya rufaa iliyokatwa na waliokuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba
na Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, kupinga adhabu ya vifungo
vya miaka mitatu jela inatolewa leo.
Jaji wa Mahakama Kuu, Projest Rugazia wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam, anatarajiwa kusoma hukumu hiyo baada ya kusikiliza hoja za
pande zote mbili.
Mahakama hiyo pia itatoa hukumu ya rufani iliyokatwa na Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP), kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu dhidi ya kina Mramba na wenzake.
Viongozi hao wa zamani kwa kupitia mawakili wao wamekata rufani
Mahakama Kuu wakipinga adhabu ya vifungo walivyopewa na Mahakama ya
Kisutu, baada ya kuwatia hatiani kwa matumizi mabaya ya madaraka kwa
kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni ya ukaguzi wa madini ya dhahabu.
Julai 6 mwaka huu, Mahakama ya Kisutu ilitoa adhabu hiyo kwa Mramba
na Yona baada ya kuwatia hatiani kwa matumizi mabaya ya madaraka na
kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7, kutokana na kutoa
msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart and Asseyers.
Katika hukumu hiyo, Mahakama ya Kisutu ilimwachia huru aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja baada ya upande
wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Mramba na Yona kwa kupitia mawakili wao wanadai kwamba adhabu hiyo
ni kubwa mno na hati ya mashtaka iliyowatia hatiani ilikuwa na
upungufu wa sheria kama ilivyobainishwa katika kifungu namba 132 cha
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Pia wanadai kwamba hapakuwapo ushahidi wa kutosha kuthibitisha mashitaka dhidi yao.
DPP anapinga adhabu waliyopewa mawaziri hao kwa madai kuwa ni ndogo.
Anadai hakimu alikosea kumuachia huru Mgonja kwa kigezo kwamba
upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake.
Pia anadai Mahakama ya Kisutu ilikosea kutowaamuru Mramba na Yona kulipa hasara ya fedha waliyoisababishia serikali.
0 comments:
Post a Comment