Baada ya kuisaidia Taifa Stars kuifunga Malawi 2-0 kwenye mechi ya
kwanza ya mchujo wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali ya Kombe la Dunia
2018,washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu, wamesema timu
hiyo ya taifa ya Tanzania itafanya maajabu kwenye mchezo wa marudiano na
kuwashangaza wenyeji wao.
Stars itarudiana na Malawi Jumapili hii jijini Blantyre katika
mchezo ambao Stars inahitaji kuepuka kipigo cha zaidi ya goli moja ili
kusonga mbele.
Wakizungumza mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo
wa juzi,washambuliaji hao wanaocheza soka la kulipwa kwenye klabu ya TP
Mazembe ya DRC, wamesema kikosi cha Stars kina uwezo wa kupata matokeo
mazuri kwenye mechi ya marudiano.
"Hakuna kinachoshindikana... hata kwao tuna uwezo wa kupata matokeo
mazuri na kuiwezesha kusonga mbele," alisema Samata aliyefunga goli la
kwanza kwenye mchezo huo.
"Msifananishe tulivyocheza dhidi ya Nigeria na leo dhidi ya Malawi,
hizi ni timu tofauti, mwalimu atafanya marekebisho tulipokosea ili
tukafanye vizuri zaidi katika mechi ya marudiani, ila tunaahidi
tutaendelea kujituma," aliongeza nyota huyo anayeshika nafasi ya pili
katika orodha ya wafungaji bora Ligi Mabingwa Afrika msimu huu akiwa na
mabao sita, moja nyuma ya kinara, Bakri Al-Madina wa El Merreikh.
Ulimwengu ambaye aliifungia Stars goli la pili, alisema kuwa
kimsingi kujiamini na kucheza kwa utulivu kutawapa matokeo mazuri kwenye
wa marudiano.
"Hatutakiwi kubweteka kwa ushindi huu, bado tuna kazi ya kufanya
kwenye mchezo wa marudiano, kikubwa ni kujiamini na kuhakikisha
tunatumia vizuri nafasi tutakazozipata," alisema Ulimwengu.
Katika mchezo huo wa juzi, pamoja na Stars kuibuka na ushindi huo
wa magoli 2-0, bado washambuliaji wake walipoteza nafasi nyingi za
kufunga, jambo ambalo kocha Boniface Mkwasa amepanga kulifanyia kazi
kabla ya Jumapili.
MKWASA AONYA
Kocha wa Stars, Mkwasa, amesema kwamba bado timu yake ina jukumu
zito la kuhakikisha inasonga mbele katika kusaka tiketi ya kucheza
fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika Russia.
Akizungumza juzi baada ya mechi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa,
Mkwasa, alisema kwamba wanajiandaa kupambana kuhakikisha wanasonga mbele
kwa sababu wanajua mechi hiyo ya marudiano itakuwa ngumu kwa vile
wapinzani wao Malawi (The Flames) watakuwa nyumbani.
"Bado tuna mlima mrefu mbele yetu, lakini tutajitahidi kutafuta
matokeo mazuri, tunajua mechi itakuwa ngumu kwa sababu wao watakuwa
wanacheza kwao, tutajipanga vizuri zaidi," alisema Mkwasa.
Aliongeza kwamba timu yake haikucheza katika kiwango kama
kilichoonekana dhidi ya Nigeria mwezi uliopita kutokana na kukosa muda
wa maandalizi mrefu na hiyo imesababishwa na wachezaji kutoka kwenye
klabu zao wakiwa na stamina zinazotofautiana.
Hata hivyo, Mkwasa ambaye Oktoba Mosi mwaka huu alipata mkataba
rasmi wa miezi 18 wa kuifundisha Stars, alisema kwamba alifurahishwa na
matokeo ya mechi hiyo ya juzi lakini hakuridhishwa na idadi ya mabao
waliyofunga.
Naye wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, amesema Stars bado ina kazi kubwa kuing'oa Malawi.
Ikiwa chini ya kocha mkuu mzawa wa kwanza tangu 2006, Stars ilipata
ushindi dhidi ya The Flames na kutanguliza mguu mmoja kutinga katika
hatua ya mwisho ya mtoano.
Hata hivyo, Malinzi anaamini kuwa Stars imefanya nusu ya kazi
inayoikabili na inapaswa kupambana kusaka matokeo mazuri katika mechi ya
keshokutwa ugenini Malawi.
"Nitumie fursa hii kuwapongeza wadau wa soka na Watanzania wote
kutokana na ushindi wa Taifa Stars wa mabao mawili dhidi ya Malawi jana
(juzi). Hata hivyo, hatupaswi kubweteka na matokeo haya, kazi bado ni
kubwa," alisema Malinzi katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam jana.
"Tumekula ng'ombe, bado kuna mkia ambao tunapaswa kwenda kuumalizia
ugenini nchini Malawi Jumapili," aliongeza kiongozi huyo huku akiweka
wazi kwamba mechi ya keshokutwa haitaonyesha moja kwa moja 'live'
kutokana na 'uchanga wa Malawi' katika masuala ya matangazo ya
televisheni.
Kikosi cha Stars kinatarajia kuondoka nchini leo kuelekea Malawi
kwa ajili ya kujiandaa kuwavaa wenyeji wao Jumapili kwenye Uwanja wa
Kamuzu Banda.
Kocha wa zamani wa timu hiyo, Mshindo Msolla, alisema kuwa Stars
ilielemewa katika safu ya kiungo hivyo Mkwasa anatakiwa kufanyia kazi
zaidi eneo.
0 comments:
Post a Comment