Mabao ya washambuliaji nyota wa TP Mazembe, Mbwana Samata na Thomas
Ulimwengu, yalitosha kuipa Taifa Stars ushindi wa 2-0 dhidi ya timu ya
taifa ya Malawi katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali kuwania kufuzu
fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi 2018 iliyochezwa kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam jana.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa kocha mkuu mpya, mzawa Boniface Mkwasa
tangu akabidhiwe mikoba Juni 21 mwaka huu na ni wa kwanza kwa timu hiyo
ya taifa ya Tanzania mwaka huu baada ya kucheza mechi 11 ikiambulia
sare na vipigo.
Mkwasa ambaye Oktoba Mosi mwaka huu alipewa mkataba wa mwaka mmoja
na nusu kuinoa Taifa Stars, anaonekana kuwa mbeleko kwa mafanikio ya
timu hiyo.
Kabla ya mechi ya jana, kocha huyo wa zamani wa Ruvu Shooting,
Twiga Stars na Yanga, aliiongoza Stars katika mechi tatu akitoa sare
mbili dhidi ya 1-1 dhidi ya Uganda na suluhu dhidi ya Nigeria na
kufungwa 2-1 dhidi ya Libya.
Taifa Stars imejiweka katika mazingira mazuri ya kusonga hatua ya
mwisho ya mchujo ambayo itamenyana na Algeria. Stars itahitaji sare ya
aina yoyote katika mchezo wa marudiano Jumapili mjini Blantyire, Malawi.
Katika mechi ya jana, Samata alifunga bao la kwanza katika dakika
ya 18 akiitendea haki krosi ya Ulimwengu kutoka wingi ya kulia iliyotua
ndani ya boksi kwa kumpiga chenga kipa Simplex Nthala kisha kuuzamisha
mpira langoni.
Dakika nne baadaye, Ulimwengu alifungala pili kwa shuti mtoto la
mguu wa kulia akiuwahi mpira uliotemwa na kipa Nthala kutokana na krosi
ya beki wa kushoto, Hajji Mwinyi Mngwali.
Malawi, ambao kipindi cha pili waliimarika zaidi kimchezo, walipata
nafasi nzuri dakika za 43, 70 na 80, lakini ubora wa kipa Ally Mustafa
‘Barthez’ na safu ya ulinzi iliyokuwa chini ya mabeki wazoefu, Shomari
Kapombe, Nadir Haroub ‘Cannavaro na Kelvin Yondani, uliwanyima nafasi ya
kupata mabao ya ugenini.
Mkwasa alisema baada ya mechi kuwa amefurahishwa na matokeo, lakini
idadi ya mabao haikumvutia kutokana na nafasi nyingi walizotengeneza.
Tanzania: Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Hajji Mwinyi, Nadir
Haroub, Kelvin Yondani, Himid Mao, Mrisho Ngassa/ Salum Telela (68),
Said Ndemla, Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu/ Ibrahim Ajibu (86) na
Farid Mussa/ Simon Msuva (80).
Malawi: Simplex Nthala, Stanley Sanudi, Mivale Gabeya, Yamkani
Fadya, Limbikani Mzava, Gerald Phiri/ Isaac Kaliati (64), Chimango
Kayira, Micium Mhone/ Mamase Chiyasa (46), Chawangiwi Kawanda, John
Banda na Robin Ngalande/ Gabadinho Mhango (58).
Matokeo mengine
Comoro 0-0 Lesotho
Shelisheli 0-3 Burundi
Mauritius 0-1 Kenya
0 comments:
Post a Comment