Vipigo vitano msimu huu, kikiwamo cha kwanza dhidi ya Simba tangu
ipande ligi kuu, vimeilazimu Mbeya City FC kuingia sokoni kusaka nyota
wanne wapya kwa ajili ya kuwajumuisha kikosini wakati wa usajili wa
dirisha mwezi ujao.
City ambayo Jumamosi ilipoteza 1-0 dhidi ya Simba, ikiwa ni mechi
ya kwanza kufungwa na mabingwa hao mara 18 wa Bara tangu ipande ligi kuu
msimu wa 2013/14, imeuanza vibaya msimu huu wa ligi kuu Bara ikiambulia
pointi nne tu kati ya 21 za raundi saba za mwanzo sawa na msimu
uliopita, ambao timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya ilipata pointi
tano pekee kwenye mechi saba za mwanzo.
Katika mahojiano maalum na Nipashe kabla ya kuanza kwa programu ya
mazoezi ya kikosi cha Mbeya City kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine
jijini hapa jana asubuhi, kocha mkuu mpya wa timu hiyo, Abdul Mingange,
alisema watasajili washambuliaji wawili, kiungo mmoja na beki wa kati
mmoja atakayeziba pengo la Juma Said 'Nyosso' aliyefungiwa miaka miwili
na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na utovu wa nidhamu.
"Tumekuwa na matokeo mabaya kutokana na kuondoka kwa nyota wetu
wengi, bado tunajenga timu, lakini lazima tupate washambuliaji wawili
wazoefu, kiungo mmoja na beki wa kati mmoja kwa ajili ya kuziba nafasi
ya mchezaji wetu aliyefungiwa na mamlaka za soka hivi karibuni
(Nyosso)," alisema meja huyo mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ).
Alipotafutwa na gazeti hili mjini hapa kuzungumzia suala hilo,
Meneja Usajili wa Mbeya City FC, Frank Mfundo, alikiri kupokea mapendezo
hayo ya kocha na kwamba tayari wameshaanza kuyafanyia kazi.
Dismas Ten, Ofisa Habari wa City, aliiambia Nipashe mjini hapa jana
kuwa mmoja kati ya nyota wanne watakaosajiliwa dirisha dogo, atatoka
nje ya mipaka ya Tanzania.
Mpaka sasa safu ya ulinzi ya City imeruhusu mabao saba katika mechi
saba zilizopita, ikiwa ni wastani wa bao moja kila mechi, huku safu yao
ya ushambuliaji ikipachika magoli matano.
Kwa mujibu wa kalenda ya matukio ya TFF, usajili wa dirisha dogo utafunguliwa rasmi Novemba 15 na kufungwa Desemba 15 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment