Kapeni za vyama vya siasa sasa zinaingia wiki ya mwisho kabla ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumapili ijayo.
Bila shaka wagombea watatumia nafasi hii kunadi sera zao ili kuvutia
wapigakura kabla ya uchaguzi huu unaotazamiwa kuwa wa kihistoria.
Ni mategemeo yetu kuwa wananchi nao watakuwa makini katika
kusikiliza sera za wagombea wanaowania uongozi wa udiwani, ubunge na
urais.
Tunachukua fursa hii kuwapongeza wagombea na wananchi kwa ujumla
kwa utulivu waliouonyesha katika kipindi chote cha kampeni zilizoanza
Agosti 22, mwaka huu.
Kumekuwa na matukio machache ya vurugu, lakini zaidi wananchi wamekuwa watulivu katika kuwasikiliza wagombea wakinadi sera zao.
Uchaguzi wa mwaka huu unatarajiwa kuwa wa kihistoria kwani kwa mara
ya kwanza kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya chama tawala CCM na vyama
vya upinzani.
Kwa mara ya kwanza tangu mfumo wa vyama vingi urudishwe, nchi yetu
inashuhudia uchaguzi wenye ushindani mkubwa zaidi. Hata hivyo, ushindani
mkali umejitokeza kwa mara ya kwanza kwa upande wa Tanzania Bara tangu
uchaguzi unaoshirikisha vyama vingi kufanyika mwaka 1995.
Tangu uchaguzi ulipofanyika kwa mara ya kwanza kwa kushirikisha
vyama vingi kwa upande wa Zanzibar kumekuwa na ushindani mkali zaidi.
Bila shaka uchaguzi huu umekuwa na ushindani mkali zaidi kutokana na sababu nyingi.
Sababu mojawapo ni rika jipya la wapiga kura, ambao wengi wao ni
vijana, wenye shauku kubwa ya kupiga kura kutokana na kukabiliwa na
changamoto mbalimbali za kimaisha.
Wapigakura hawa wapya wanataka mabadiliko katika maisha yao, jambo
ambalo limekuwa likipigiwa kampeni na wagombea wa vyama vyote.
Hata hivyo, wananchi walio wa kawaida nao wana shauku kubwa ya
kushiriki uchaguzi huu wakiamini kuwa itakuwa fursa nzuri ya kuchagua
viongozi watakaoendeleza gurudumu la maendeleo.
Ni dhahiri wananchi wanataka viongozi watakaokuwa na uwezo wa
kukabiliana na matatizo ya taifa letu na hasa yale ya kupambana na
umasikini, rushwa, ufisadi na ukosefu wa ajira. Tunashauri wananchi
kuhakikisha kuwa wanatumia vizuri kipindi hiki kilichobaki kuchagua
viongozi makini wa kukabiliana na matatizo ya taifa letu.
Ni vizuri sasa Watanzania kutumia vizuri kipindi hiki kilichosalia
kuhakikisha wanawapima na kuwachambua wagombea wa nafasi mbalimbali za
uongozi.
Watanzania wanapaswa kuwa macho na watu wanaowania nafasi hizi za uongozi kwa ajili ya kujinufaisha.
Mathalani, kuna imani kuna watu wanaowania ubunge kwa fikra kuwa
wakifika huko watanufaika kutokana na posho mbalimbali watakazozipata.
Ndiyo maana kuna wengine hufikia hatua ya kumwaga mamilioni ya
fedha kwa kuwahonga wapigakura ili wafike bungeni kunufaika na fedha
hizo.
Yafaa kuelewa kwamba fursa hii adhimu isipotumika vema kwa
kuwachagua viongozi wanaofaa, basi tutaendelea kuwa nao hadi miaka
mitano ijayo utakapofanyika uchaguzi mkuu mwingine.
Ni kwa msingi huo basi ndipo tunawasihi Watanzania kuhakikisha
kwamba wanatumia akili na utashi waliopewa na Mwenyezi Mungu kuwachagua
viongozi wanaofaa ambao watalisukuma mbele gurudumu la maendeleo la
Taifa letu.
0 comments:
Post a Comment