KIKOSI cha wachezaji 20 wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars,
kinaondoka leo kwenda Malawi kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya
The Flames kwa ajili ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa
Dar es Salaam, Taifa Stars iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na hivyo
kujiweka katika nafasi nzuri ya kucheza hatua inayofuata.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa alisema kuwa pamoja na
ushindi huo wa mabao 2-0 lakini wanatarajia kupata upinzani mkali katika
mchezo huo wa marudiano.
Alisema Malawi ni timu nzuri pamoja na kuwafunga na wanatarajia
upinzani mkali kutoka kwa wenyeji hao katika mchezo huo wa marudiano.
Mkwasa alisema kuwa timu yake ingeweza kuibuka na ushindi mnono zaidi
kama wachezaji wake wangekuwa na uzoefu wa mechi za kimataifa.
Alisema kuwa muda wa maandalizi ni mdogo kwa ajili ya mechi hiyo ya
marudiano kwani jana wachezaji wake walikuwa mapumzikoni jana na leo
wanaondoka kwenda Malawi.
Alisema pamoja na uchache wa muda lakini watajitahidi mara baada ya
kufika kuanza mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo
huo wa Jumapili. Aidha, Mkwasa alitaka wachezaji wake kupatia mazoezi
zaidi ya mechi za kimataifa za majaribio ili waweze kupata uzoefu wa
mechi hizo.
Tofauti na ilipokuwa ikitaka kucheza na Nigeria katika mchezo wa
kufuzu kwa Mataifa ya Afrika (Afcon), Stars ilipiga kambi ya zaidi ya
wiki moja nchini Uturuki na kutoka suluhu na mabingwa hao wa zamani wa
Afrika.
Alisema kuwa timu yake ilikosa nafasi nyingi za kufunga kwa sababu ya
kutokuwa na uzoefu wa kutosha na kama wangekuwa na uzoefu bila shaka
wangeweza kuibuka na mabao ya kutosha. Hatahivyo, Mkwasa hakutaja
wachezaji wanaoondoka leo lakini alisema kuwa Ofisa habari wa Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto angetuma majina hayo.
Lakini hadi tunakwenda mitamboni hakutuma majina hayo. Taifa Stars
ikiitoa Malawi hatua inayofuata itacheza na Algeria inayoshika nafasi ya
kwanza kwa ubora Afrika.
0 comments:
Post a Comment