Mfumuko wa bei ni janga kubwa. Tafsiri yake tu inatosha kuonesha namna
ambavyo hatupaswi kuuchekea. Kama taifa, tunateseka leo kwa sababu ya
kushindwa kuudhibiti. Wananchi wa chini wanaangamia.
Maana yake ni kupanda kwa gharama za maisha. Bei za vitu na huduma
muhimu za kijamii zinakuwa juu. Wakati mwingine ni matokeo ya kushuka
thamani ya sarafu. Ulegevu wa benki kuu au udhaifu wa wizara ya fedha na
uchumi katika usimamizi wa utekelezwaji wa bajeti, kwa tafsiri
iliyooka, ndiyo kitovu cha tatizo.
Ni mpanga bei anayepitiwa na msemo “mwenye shibe hamkumbuki aliye na
njaa” ndiye peke yake anayeweza kuona bei hizi ni rahisi. Watanzania
wanateseka, kuendelea kuwapandishia gharama za maisha ni kuzidi
kuwaumiza na kuwakatisha tamaa.
Mfumuko wa bei ukiendelea kuitesa nchi, ajabu ni kwamba Gavana wa Bot,
Benno Ndulu bado yupo palepale. Ufanisi wake hauonekani katika kuhakisha
benki kuu kama roho ya nchi, inafanya kile kinachotakiwa kuhakikisha
gharama za vitu muhimu na huduma nyeti hazipandi.
Taarifa kwamba mfumuko wa bei umefikia asilimia 20, inatoa picha kuwa
Bajeti ya Serikali ya mwaka 2015-2016, imepunguza uwezo wa kununua
bidhaa na huduma kwa takribani asilimia 6. Hii ni sawa na shilingi
trilioni moja kuyeyuka kabla hata mwaka mpya wa fedha haujafika.
Hali ni mbaya zaidi kwa wananchi, kwani mfumuko wa bei za vyakula umekua
kwa kasi kikubwa mno. Ofisi ya Takwimu ilishaonesha kuwa mfumuko wa bei
za chakula pekee umepaa kwa wastani wa asilimia 25. Upande huo kukiwa
bado majanga, nauli nazo zinaongezeka.
Hata hivyo, ukiangalia kwa undani zaidi, utakuja kugundua kuwa bei za
chakula zimekuwa maradufu, ukilinganisha na hali ilivyokuwa miaka miwili
iliyopita. Mchele, sukari, nyama, samaki, sembe na ngano, vyote
vimepanda kwa kati ya asilimia 30 mpaka 50.
Gesi ipo juu, mafuta ya taa yalishapanda kwa asilimia 71 mpaka 75 tangu
miaka miwili iliyopita. Hii inasababisha wengi wakimbilie nishati ya
mkaa ambayo ni hatari, ingawa nako huko ni pagumu kwa mwananchi wa
kawaida, kwani umepanda kwa asilimia 30.
Mfumuko wa bei unasukuma Watanzania wengi zaidi kwenye dimbwi la
umasikini, unapunguza uwezo wa serikali kutoa huduma za kijamii kupitia
bajeti na hata kutimiza mipango ya miradi ya maendeleo kama miundombinu
ya barabara, umeme, bomba la gesi, madaraja nk. Mkakati mahususi
unatakiwa kubadili hali hii.
Kwa namna tunavyokwenda, kama tusipochukua hatua, kuna hatari ya dhahiri
kwamba tunaweza kurejea mfumuko wa bei wa mwaka 1992 ambao ni asilimia
22, kadhalika tunaweza kuukaribia ule uliokuwa tishio zaidi, wa mwaka
1994, asilimia 33.
Kwa nini Ndulu anastahili lawama na kuwajibishwa kwa hili? Siku zote
kuna njia mbili ambazo husimamiwa na benki kuu katika kudhibiti mfumuko
wa bei. Mojawapo ni Monetary Measures, hii hugusa moja kwa moja sera
kuhusu uchumi ndani ya benki kuu kwa kuweka riba kubwa dhidi ya mabenki
ya kibiashara ili kuifanya serikali (hazina) kuwa na akiba nzuri.
Bot lazima isimamie sera ya riba ili kusababisha kupanda kwa gharama za
kukopa dhidi ya mabenki ya kibiashara kutoka benki kuu. Matunda yake ni
kupungua kwa mtiririko wa fedha kwa wananchi, hilo likifanikiwa serikali
itaweza kupanga bei za bidhaa kulingana na hali za wananchi. Hivi sasa
fedha zipo nje, wafanyabiashara wana hela sana, kwa hiyo inakuwa vigumu
kuwadhibiti.
Mfumuko wa bei kwa tafsiri nyingine ni matokeo ya wafanyabiashara
kuizidi nguvu serikali, kwa hiyo wanajipangia bei bila kupingwa. Ndullu
kwa nafasi yake, anatakiwa kuhakikisha sera zinafanya kazi, serikali
inakuwa na nguvu siku zote dhidi ya wafanyabiashara. Bot ikiendelea
kusinzia, stori zitabaki zilezile.
0 comments:
Post a Comment