Tangu kuanza kwa kampeni Agosti 22, mwaka huu, tumewasikia wagombea
wa nafasi mbalimbali za uongozi wakinadi sera zao na kutoa ahadi lukuki
watakazotekeleza iwapo watachaguliwa.
Wagombea wengi wamekuwa wakijikita zaidi kuzungumzia sekta za gesi,
mafuta, madini, ajira, ufugaji, viwanda na kadhalika, huku sekta ya
kilimo ikiachwa ama kuelezwa kwa kifupi mno licha ya kwamba ndiyo uti wa
mgongo wa uchumi wa Taifa.
Ni dhahiri kwamba kilimo mbali ya kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa, lakini pia ndiyo mwajiri mkubwa
wa Watanzania kutokana na ukweli kwamba zaidi ya asilimia 75 ya
wananchi hususan vijijini, wanategemea sekta hiyo kuendesha maisha yao
ya kila siku.
Ukweli utazidi kubaki pale pale kuwa kilimo kina fursa ya kuendelea
kuwa uti wa mgongo wa Taifa letu kwa kuwa ndiyo sekta inayotuhakikishia
chakula na biashara kwa mazao ya biashara kama pamba, kahawa, korosho,
karafuu, pareto, tumbaku na kadhalika.
Kwa bahati mbaya, baadhi ya wagombea hawajaipa msukumo wa kutosha
kwenye kampeni zao na badala yake wamekuwa wakiwaahidi vijana kuwa
watatengeneza fursa za ajira bila kuwaeleza ukweli kwamba ajira nambari
moja ni kilimo.
Hakuna asiyefahamu kwamba baadhi ya vijana ambao ndiyo nguvu kazi
kubwa ya Taifa, wamekuwa wakiranda randa mitaani kwa maelezo kuwa hawana
ajira huku mamilioni ya ekari tena zenye rutuba nzuri, zikibaki mapori!
Tulidhani kwamba wakati huu wa kampeni, vyama vingejikita katika
kuwaelimisha vijana na Watanzania kwa ujumla kwambanjia sahihi ya
kujikwamua kiuchumi, ni kilimo na ndiyo tegemeo kubwa la uchumi wa
Taifa.
Ni vema wagombea mbali ya `kupiga siasa,' lakini pia wakaweka
bayana tena bila kumung'unya maneno kwamba tegemeo kubwa la uchumi wa
Taifa, ni kilimo, kilimo, kilimo.
Basi ni wakati mwafaka sasa kwa kila mgombea akaelezea mikakati ya
chama chake iwapo kitaingia madarakani kitakabilianaje na changamoto
nyingi zinazowakabili wakuliwa wa Tanzania.
Hata hivyo, wapo baadhi ya wagombea wamethubutu kuzungumzia
watafanya nini kama watashinda kukabiliana na changamoto zinazowakabili
wakulima kama kukopwa mazao yao, ucheleweshaji wa pembejeo, kilimo cha
jembe la mkono, kuyataja baadhi. Hawa tunawapongeza, lakini tunasema
haitoshi.
Kwa miaka mingi, wakulima wa Tanzania wamekuwa wakiendesha kilimo
cha bora mkono uende kinywani badala ya kilimo cha kibiashara.
Kilimo cha jembe la mkono na bila matumizi sahihi ya mbolea, kamwe hakitawatoa wakulima wa Tanzania kutoka hapa walipo.
Hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete, alisisitiza kuwa umefika wakati
kilimo kurudishwa kwenye hadhi yake na kwamba upatikanaji wa pembejeo,
ndiyo uti wa mgongo wa sekta hii.
Rais Kikwete aliyasema hayo alipokuwa akizindua kiwanda kikubwa cha
mbolea (Fertilizer Terminal) jijini Dar es Salaam kilichojengwa na
kampuni ya kilimo ya kimataifa ya Yara kutoka nchini Norway kwa gharama
ya Sh. bilioni 50.
Imeelezwa kwamba kituo hicho chenye uwezo wa kuhifadhi tani 45,000
za mbolea kwa wakati mmoja, ni kikubwa kuliko vyote barani Afrika.
Moja ya pembejeo muhimu kwa mkulima ni mbolea, hivyo tunawasihi
wagombea katika siku chache hizi za kampeni zilizosalia, kuelekeza nguvu
zao kuelezea namna vyama vyao vilivyojipanga kulikwamua Taifa kupitia
sekta ya kilimo.
0 comments:
Post a Comment