Image
Image

DAKTARI John Magufuli ameapishwa rasmi kuwa Rais wa Awamu ya Tano Tanzania.


DAKTARI John Magufuli ameapishwa rasmi kuwa Rais wa Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sherehe zilizofana zilizofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Dar es Salaam jana.

Dk Magufuli (56) anachukua nafasi hiyo ya Urais kutoka kwa Rais aliyemaliza muda wake, Jakaya Kikwete baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni.

Katika sherehe hizo zilizofana kwa kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi ambao wengine walilazimika kupelekwa kwenye Uwanja wa Taifa baada ya wa Uhuru kufurika, pamoja na wageni kutoka nchi za nje, Dk Magufuli aliapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman.

Aidha, kabla ya kuanza kwa sherehe hizo uwanjani hapo, kulinyesha mvua kubwa huku jua likiwaka kidogo, ishara ambayo kwa mujibu wa wazee waliokuwepo uwanjani hapo, ni nyota njema ya kiongozi ajaye.

Awali kabla ya kiapo hicho, Jaji Chande pamoja na Spika wa Bunge, Anne Makinda waliongoza maandamano rasmi kuelekea kwenye jukwaa la kiapo, yakiwahusisha pia Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju na Jopo la Majaji.

Wengine walioshiriki katika maandamano hayo ni wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama akiwemo Mkuu wa Majeshi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange, viongozi wa madhebu ya dini ambao ni Shekhe Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zuberi, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa.

Aidha, katika maandamano hayo pia yaliwashirikisha wazee wawili kutoka Tanzania bara ambaye ni Balozi Job Lusinde na kutoka Tanzania Visiwani, Shekhe Ally Hemed Bakari. Baada ya maandamano hayo, Makamu wa Rais aliyemaliza muda wake, Dk Mohamed Gharib Bilal na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, nao walipanda katika jukwaa hilo la kiapo.

Ilipofika saa 4.22, Dk Magufuli pamoja na Samia Suluhu Hassan ambao walishinda urais huo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliandamana kwenda jukwaani hapo kwa ajili ya kiapo.

Saa 4.47 asubuhi, Jaji Chande alimuapisha rasmi Dk Magufuli kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo baada ya kiapo hicho, Rais huyo alikabidhiwa rasmi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kiapo hicho, Dk Magufuli aliapa kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Mimi John Pombe Magufuli, naapa kwamba nitafanya kazi zangu za Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uaminifu, bidii na moyo mkunjufu. Nitatenda haki kwa Watanzania wote bila woga, upendeleo wala chuki, Mwenyezi Mungu nisaidie,” aliapa Rais Magufuli.

Aidha, aliendelea kuapa kuwa atatekeleza madaraka aliyopewa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muda mfupi kabla ya kuapa, Mpambe wa Rais (ADC), alihama kutoka kwa Rais Kikwete, akimuaga kwa kumpigia saluti na kisha kupeana naye mkono, na kisha akahamia nyuma ya Dk Magufuli wakati akijiandaa kula kiapo.

Akiwa jukwaani hapo, Rais Dk Magufuli aliketi kwenye kiti cha jadi na kukabidhiwa ngao na mzee aliyewakilisha Tanzania Bara ambaye ni Balozi Lusinde na mkuki alikabidhiwa na mzee anayeiwakilisha Tanzania Visiwani, Shehe Bakari.

Katika sherehe hizo, pia Jaji Chande alimuapisha rasmi Makamu wa Rais, Samia na kumkabidhi Katiba ya Tanzania. Samia anaweka historia Tanzania ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo wa pili wa juu Tanzania.

Baada ya kiapo hicho, kilichohitimishwa kwa dua ya kuliombea Taifa la Tanzania kutoka kwa viongozi wa dini ambao ni Mufti Zuberi, Kardinali Pengo na Askofu Malasusa, Dk Magufuli alikabidhiwa rasmi madaraka na Rais Kikwete aliyetoka nje ya uwanja wa Uhuru na baadaye kurejea tena.

Rais Magufuli baada ya kukabidhiwa madaraka, alipanda jukwaa la saluti kwa ajili ya kupokea salamu ya heshima kutoka kwa gwaride la kijeshi uwanjani hapo, ambapo pia alipigiwa mizinga 21 na bendera ya Rais kupandishwa, ishara ya mwanzo wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Aidha, baada ya bendera kupandishwa na mizinga kukamilika kupigwa, alikagua rasmi gwaride hilo kwa mwendo wa pole, ambalo askari wake walijipanga katika umbo la Alpha, ikiwa ni ishara ya mwanzo wa utawala wake akiwa kama Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Tanzania.

Alionesha ukakamavu wakati akikagua gwaride. Baada ya ukaguzi huo akiwa Rais wa Tanzania, Dk Magufuli alikwenda jukwaa kuu huku wananchi wakimshangilia na baada ya kuketi, gwaride lilipita mbele yake kwa heshima, tukio lililoambatana na kupita kwa ndege za kivita kwa mbwembwe na kuinamisha bawa moja, ishara ya kutoa heshima kwa Rais huyo.

Tukio hilo la kuapishwa kwa Rais Dk Magufuli lilihitimishwa kwa wimbo maalumu wa kumkaribisha madarakani, lakini pia kumuaga Rais aliyemaliza muda wake, Kikwete. Dk Magufuli baada ya kiapo hicho, anakuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano baada ya kuwabwaga kwa kura, washindani wake katika uchaguzi uliomalizika hivi karibuni nchini.

Mgombea huyo wa CCM alipata ushindi wa asilimia 58.46 wakati mshindani wake wa karibu, Edward Lowassa alipata asilimia 39.97. Katika hotuba yake ya shukrani, Dk Magufuli amesema analo deni kubwa kwa Watanzania katika kutimiza ahadi alizoahidi na amesisitiza Umoja wa Kitaifa ili kuwezesha Watanzania wote kushiriki katika ujenzi wa taifa lao.

Aidha, ameahidi kufanya kazi na viongozi wa vyama vya upinzani kutokana na kile alichosema hawakuwa wapinzani, bali washindani wake huku wote kwa pamoja wakiwa na lengo la kuijenga Tanzania.

“Natambua ninalo deni kubwa kwa Watanzania. Nimejifunza mengi wakati nikitembea maeneo mbalimbali nchini kuomba kura. Nitumie nafasi hii kuwaomba Watanzania wote tumuombe Mungu ili ahadi zote tulizozitoa wakati wa kampeni ziweze kutekelezeka kwa kipindi kifupi. “Nawahakikishia nimepokea dhamana hii nikielewa changamoto zilizopo na hivyo naahidi kuwa nitafanya kazi kwa juhudi ili kuhakikisha kuwa tunaliletea Taifa letu maendeleo,” alisema Dk Magufuli ambaye anakuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania akimrithi Rais Jakaya Kikwete aliyemaliza muda wake kikatiba jana.

Akizungumzia umuhimu wa kujenga umoja wa kitaifa baada ya kumalizika kwa uchaguzi, Dk Magufuli alisema yupo tayari kufanya kazi na vyama vya upinzani nchini na alitumia fursa hiyo kuwaomba waliokuwa wagombea saba wa nafasi ya urais kumpa ushirikiano kwa vile sasa ndiye Rais rasmi wa Tanzania.

“Naomba nikiri kwamba nimejifunza mengi kutoka kwa wagombea wenzangu na nitayafanyia kazi. Napenda niseme wazi kwamba wagombea wale saba hawakuwa wapinzani wangu, bali walikuwa washindani wangu lengo likiwa ni moja nalo ni kuijenga Tanzania. “Uchaguzi sasa umekwisha na Rais ni John Pombe Joseph Magufuli, kilichopo mbele yetu sasa ni kazi tu kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Ushindi wangu ni ushindi wa Watanzania, sote tushikamane tuijenge nchi yetu. Nchi ni kubwa kuliko vyama vyetu,” alisema Dk Magufuli huku akirejea kaulimbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ ambayo ilikuwa maarufu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Kwa upande wa suala la Zanzibar, alitaka kuwapo kwa kuvumiliana akisema kuwa ni kipindi cha majaribu, wakati huu ambao viongozi wanatafuta suluhu ya mgogoro wa uchaguzi visiwani humo.

Katika hatua nyingine, Rais aliipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuratibu Uchaguzi Mkuu kwa uhuru na uwazi pamoja na kuwepo kwa kasoro ndogo ndogo. Alivipongeza pia vyombo vya ulinzi na usalama na vyombo vya habari kwa kazi kubwa vilivyofanya wakati wa uchaguzi huo ambao ulifanyika kwa amani na utulivu.

Kuhusu Bunge jipya, Rais aliahidi kushirikiana kwa nguvu zake zote na wabunge waliochaguliwa katika uchaguzi wa hivi karibuni bila kubagua vyama wanavyotokea kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Watanzania huku pia akiahidi kutoa mwelekeo wa serikali yake siku chache zijazo.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment