Mazungumzo hayo yaliyowajumuisha viongozi watano wa kitaifa akiwamo
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais,Maalim Seif Sharif Hamad, yalichukuwa takriban saa sita.
Mazungumzo hayo yalianza saa 4:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni huku
kukiwa hakuna taarifa zozote zilizopatikana kilichofikiwa katika
mazungumzo hayo.
Bado vikao hivyo vya mazungumzo vimekuwa na usiri mkubwa licha ya
kuenea kwa taarifa zisizo rasmi na mitaani zimepewa jina la `Dripu.'
Viongozi wengine walihudhuria mazungumzo hayo jana ni Marais
wastaafu Amani Abeid Karume, Ali Hassan Mwinyi na Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Vikao hivyo vimekuwa na usiri mkubwa ambapo hata viongozi wa vyama
vikuu vya siasa vinavyohusika na mgogoro wa uchaguzi Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na Chama Cha Wananchi (CUF), vimeeleza havielewi kilichozungumzwa
ndani ya vikao hivyo.
Chanzo cha kuzuka mgogoro huo ni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta uchaguzi uliofanyika
Oktoba 25, mwaka huu kwa madai kuwa haukuwa wa huru na haki.
CCM: Hatujaridhia Maalim Seif kuapishwa.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimekanusha habari zilizosambazwa
katika mitandao ya kijamii kuwa kimeridhia mgombea urais wa visiwa hivyo
kupitia Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad, kuapishwa kuwa Rais wa
Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Naibu Katibu
Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema taarifa
zinazosambazwa mitandaoni na kumnukuu yeye akisema kuwa CCM imeridhia
Maalim Seif apewe urais ni uongo kwani hakuna kitu kama hicho.
Alisema suala la kurudiwa uchaguzi ni jambo la lazima baada ya
matokeo ya uchaguzi mkuu kufutwa na kutangazwa rasimi katika Gazeti la
Serikali la Novemba 6, mwaka huu kama sheria inavyotaka.
Vuai alisema mshindi wa uchaguzi wa Zanzibar ataapishwa na kuwa
Rais baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio na siyo vinginevyo na
kuwataka wananchi kupuuza taarifa za uongo zinazosambazwa katika
mitandao ya jamii kwa malengo maalum.
Vuai alisema CCM imechukua hatua za kuripoti katika vyombo vya
sheria ili watu waliosambaza uzushi huo katika mitandao ya jamii wasakwe
na kuchukuliwa hatua za sheria.
0 comments:
Post a Comment