Taarifa hiyo inatokana na maelekezo yaliyotolewa jana na serikali
kupitia kwa Msajili wa Hazina, Lawrance Mafuru, aliyewaambia wakuu wa
taasisi na mashirika ya umma kwenye mkutano wao jijini Dar es Salaam
jana kuwa ni vyema wakaongeza tija na ufanisi katika utendaji wao na
kwamba, pale inapodhihirika kuwa wapo wafanyakazi wengi wasiolingana na
uzalishaji wa taasisi au shirika husika, ni vyema baadhi yao
wakapunguzwa.
“Kuna kampuni ambazo zimepewa mtaji na serikali, lakini zinashindwa
kuzalisha. Zinaandika barua kuomba msaada Serikali Kuu. Kama unaona
(mkuu wa taasisi) una wafanyakazi wengi na huzalishi kwa namna
inayotarajiwa, ni vyema upunguze watu,” alisema Mafuru.
Kadhalika, licha ya kutoa maelekezo hayo, Mafuru alizitaja taasisi
kadhaa zinazoendeshwa kwa hasara au kuzalisha chini ya kiwango
kinachotarajiwa kuwa ni Tanesco, Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia
(Tazara), Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Shirika la Ndege (ATCL),
Kampuni ya Simu Tanzania ( TTCL) na Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Maafuru alizitaja taasisi na mashirika mengine yasiyofanya vizuri
kuwa ni Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Mamlaka ya Bandari
(TPA), Kampuni ya Miliki ya Rasilimai za Reli (Rahco) na Chuo cha
Usimamizi wa Fedha (IFM).
Mafuru alisema Serikali haihitaji kuvuna fedha katika taasisi hizo,
bali jambo kubwa ni kuona kuwa zinajiendesha na kutimiza malengo
yanayotarajiwa na umma wa Watanzania.
“Serikali haihitaji kuchukua fedha katika taasisi hizi. Isipokuwa
tunataka (taasisi za umma) zifanye kazi na ziwe nguzo za uchumi wa nchi.
Tuache bajeti inayotengwa (na serikali) ifanye kazi nyingine ya
maendeleo kwa Watanzania,” alisema, huku akiyataja Tazara na TRL kuwa ni
vinara wa kuomba fedha kwa Serikali Kuu ili kulipa mishahara ya
wafanyakazi wake.
“Kwa mfano Tanesco, kwa kipindi chote ilichoanza kufanya kazi mpaka
sasa tulitarajia iwe imefanya kazi nzuri ya uzalishaji, lakini badala
yake tunaona kinyume chake na hapo isitegemee kwamba endapo itaendelea
kufanya hivyo serikali itakuwa inaangalia tu,” alisema.
“Ni vema kama kuna shirika au taasisi ya umma ambayo inaona
haizalishi na ina wafanyakazi wengi iwapunguze wafanyakazi hao. Kama
tunaona tunashindwa, ni vyema tupunguze watu au turudi nyumbani
tukapumzike,” alifafanua Mafuru.
Mafuru aliongeza kuwa baadhi ya sababu za kufanya vibaya kwa
taasisi na mashirika ya umma ni uzembe wa baadhi ya watumishi ambao
hawafanyi kazi kwa kiwango kinachotarajiwa na wala kuwajibika ipasavyo
katika kutimiza majukumu yao.
Alisema tatizo jingine ni viongozi wa baadhi ya taasisi na
mashirika hayo ya umma kuchukulia nafasi za uteuzi wanazopewa kuwa ni
zawadi, fikra ambazo hivi sasa wanapaswa kuzifuta mara moja na
kutanguliza zaidi uwajibikaji hasa kwa kutambua kuwa serikali ya awamu
ya tano inaangalia zaidi utendaji wenye matokeo chanya kwa umma na siyo
kinyume chake.
“Msifikiri kwamba nyie ndiyo wapishi (wajuzi) pekee… wapo watu
wengine wanaojua zaidi, kwa hiyo mjiandae kufanya kazi. Kila mtu
atawajibika kwa nafasi yake,” alisema.
ASHANGAA KWA NINI HASARA?
Alisema ni pamoja na kwamba serikali imezipa mali taasisi hizo
kujiendesha, lakini zimendelea kuwa mzigo kwa serikali kwani baadhi
hushindwa kuzalisha na kuwa vinara wa ‘kutembeza bakuli’ kwa maana ya
kuomba msaada kwa Serikali Kuu mara kwa mara.
Mafuru alikitaja Chuo cha IFM kuwa ni mojawapo ya taasisi za
serikali zinazoshangaza kwani licha ya kuwa na fursa ya kuzalisha, bado
kimekuwa kikiendeshwa kwa hasara na kuwa miongoni mwa vinara wa kuomba
msaada kwa Serikali Kuu.
“Kwa mfano Chuo Kikuu binafsi cha Tumaini, kinajiendesha kutokana
na ada za wanafunzi pekee. Kwa nini IFM inashindwa kufanya hivyo?”
alihoji.
Alisema taasisi zinazojiendesha kwa hasara zimekuwa mzigo mzito kwa
serikali, hivyo ni lazima sasa kwa wakuu wa taasisi husika kuhakikisha
kuwa wanaongeza ufanisi ili kujikwamua kutoka katika hali mbaya kiuchumi
waliyonayo.
“Hivi sasa serikali ina taasisi 220 kutoka 600 zilizokuwapo awali.
Pamoja na kwamba taasisi za serikali zimepewa assets (mali) za
kuzalisha, bado (baadhi) zimeshindwa kufanya hivyo, badala yake nyingine
kila siku zinaandika barua kuomba fedha katika Mfuko Mkuu wa Serikali
kuongezewa mtaji,” alisema.
BANDARI NAKO UTATA
Katika hatua nyingine, Mafuru alisema inasikitisha kuona kuwa
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ni miongoni mwa taasisi zisizozalisha
kwa kiwango kinachotarajiwa na kwamba hadi sasa, hakuna faida yoyote
ambayo imekuwa ikirudisha serikalini.
Alisema kama TPA inafanya vizuri, ilitakiwa kufanya maendeleo mengine ikiwamo kujenga bandari nyingine.
Aliitaka taasisi hiyo na nyinginezo kama TPDC kujifunza kutoka kwa taasisi binafsi juu ya namna ya kuongeza uzalishaji.
Alisema kutokana na uendeshaji wa hasara kwa baadhi ya taasisi na
mashirika ya umma, matokeo yake mashirika na taasisi hizo, kwa pamoja
huchangia asilimia 22 tu ya pato la Taifa kwa mwaka, hali ambayo
haipaswi kuendelea.
RIPOTI YA UKAGUZI
Wakati huo huo, Mafuru alitoa agizo kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kuwasilisha ripoti ya ukaguzi wa taasisi za
umma ifikapo Desemba 15, zikiwamo zote zilizobainika kuwa hazikuwa
zikifanyiwa ukaguzi hapo kabla.
0 comments:
Post a Comment