CHAMA cha siasa cha Alliance for Tanzania Farmers (AFP) kimetoa
pongezi kwa Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kasi
ya utendaji kazi ambayo wameionesha na kuleta matumaini kwa wananchi.
Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam
mwishoni mwa wiki, viongozi wa chama hicho walisema kasi aliyoanza nayo
Dk Magufuli ndio kasi ambayo wananchi wengi walikuwa wakiitamani siku
zote.
“Watanzania walio wengi wamefurahishwa sana na maamuzi mbalimbali
ambayo Rais amekuwa akiyatoa hasa kufuta safari za nje pamoja na kufuta
baadhi ya maadhimisho ambayo yalikuwa yakitumia fedha nyingi za umma
huku wananchi wakiteseka,” alisema Mkurugenzi wa Mahusiano na Makundi
Maalumu wa AFP, Peter Sarungi.
Sarungi alisema maamuzi ya Rais kufuta safari za nje zisizo na tija
kwa taifa pamoja na matamasha na maadhimisho mbalimbali yataleta ufanisi
kwa watendaji wa serikali na kuwafanya wananchi kuwa na matumaini
mapya.
Alisema Dk Magufuli anaishi katika maneno yake ambayo alikuwa
akiyazungumza kipindi cha kampeni na sasa anayafanyia kazi kwa vitendo
jambo ambalo ni faraja kwa walio wengi.
“Watanzania tulio wengi tupo nyuma yake na huyu ndio aina ya kiongozi
ambaye tulikuwa tunamtaka ili tufikie tunapotaka,” alisema Sarungi.
Aidha, Sarungi alisema mbali na kuwapongeza viongozi hao, lakini pia
walimtaka Waziri Mkuu Majaliwa kukabiliana na changamoto mbalimbali
zilizopo chini ya ofisi yake.
Miongoni mwa mambo waliyotaka kufanyiwa kazi ni kuboresha na kuandaa
mikakati mipya ya kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), kwa kuiongezea makali ikabiliane na rushwa nchini.
Upande wa Rais, alisema akasimamie vyema afya za watu wenye ulemavu,
wazee, wanawake na watoto zinaboreshwa kwa kiwango cha juu na
kuhakikisha anakomesha mauaji ya albino na vikongwe.
Mbali na hayo, viongozi hao AFP chenye makao makuu yake visiwani
Zanzibar, walisema Dk Magufuli ahakikishe Tanzania Bara na Zanzibar
zinabaki na umoja wao kwa kudumisha Muungano.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment