Katika
sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Tanzania zilizofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru,
Dar es Salaam jana, Kikwete aliwasili hapo saa 4.23 asubuhi akiwa kwenye gari
la wazi, huku akisindikizwa na pikipiki 12 za askari wa Kikosi cha Usalama
Barabarani, alizunguka uwanja huo huku akiwapungia wananchi mkono na kuwaaga.
Baada ya
kukamilisha mzunguko huo ambao ulizua hamasa na nderemo kutoka kwa wananchi
waliohudhuria sherehe hizo, Rais Kikwete alikwenda moja kwa moja kwenye jukwaa
la saluti, ambako alipokea salamu ya heshima na kupigiwa mizinga 21
iliyoambatana na Wimbo wa Taifa.
Aidha,
baada ya tukio hilo, gwaride la kijeshi lililokuwapo uwanjani hapo, lilijipanga
katika umbo la Omega, ambalo ni herufi ya mwisho ya Kigiriki ikiwa na maana ya
mwisho.
Gwaride
hilo likiwa katika umbo hilo, Rais aliyemaliza muda wake, alilikagua na kisha
kurejea kwenye jukwaa la saluti ambako alipokea tena salamu ya heshima na
bendera ya Rais kushushwa, ikiwa ni ishara ya kuvua madaraka na kumaliza muda
wake wa uongozi kama Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Pia,
baada ya tukio hilo la bendera kushushwa, Rais huyo aliaga rasmi kwa kuvua
madaraka yake ambapo alitoka uwanjani hapo saa 4.50 kupitia gari la wazi na
kutoka nje ya uwanja huku akiwapungia mkono wa kwa heri wananchi waliohudhuria
uwanjani hapo.
Alirejea
baadaye kupitia mlango wa chini ya jukwaa kuu. Katika hali isiyo ya kawaida,
wengi wa wageni waliohudhuria sherehe hizo, walionekana kuguswa na tukio hilo
la Rais Kikwete kuaga kwani pamoja na kumpungia mkono, baadhi yao walionekana
wakifuta machozi, ishara ya huzuni ya kumuaga Rais waliyemzoea na kumkaribisha
Rais mpya, Dk Magufuli.
Aliporejea
jukwaani, alisalimiana na wageni mbalimbali na alipomfikia mkewe Mama Salma
Kikwete, alimkumbatia na kwa pamoja waliwapungia mkono wa kwa heri, wananchi na
viongozi waliokuwepo uwanjani hapo, na baadaye aliketi kiti cha pembeni ya Rais
mpya, Dk Magufuli.
Baada ya
sherehe, Kikwete aliondoka uwanjani hapo akitanguliwa na Rais mpya Dk Magufuli,
na kabla ya kuingia ndani ya gari lake, alitumia fursa hiyo, tena kuwapungia na
kuwaaga wageni na wananchi waliokuwepo uwanjani ambao walimshangilia na
kumpungia pia mkono.
0 comments:
Post a Comment