Hakuna
ubishi kwamba ulipitia safari ndefu yenye milima na mabonde hadi kufikia hatua
hii ya kuwa mfanyakazi nambari moja wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Mliowania
nafasi hiyo kupitia chama chako, Chama Cha Mapinduzi (CCM) mlikuwa 38 lakini
hatimaye wewe ndiye uliyeibuka kuwa mshindi wa kupeperusha bendera ya CCM
katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi hiyo na wagombea wengine saba kutoka
vyama vya upinzani.
Mkaingia
kwenye mchakato wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuteuliwa rasmi kuwania
nafasi hiyo, mkaanza kampeni zilizokuwa na ushindani wa hali ya juu kuliko
chaguzi nyingine nne za vyama vingi zilizopita.
Kura
zikapigwa na hatimaye ukaibuka mshindi, ukakabidhiwa cheti cha ushindi na
kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mambo
hayo yote yalifanyika kwa uwazi, umakini na kwa amani na usalama wa hali ya juu
kiasi cha sisi kama Watanzania kusikia wenzetu wa nchi mbalimbali waliotuma
waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa kupitia taasisi na mashirika mbalimbali ya
ndani na nje ya Tanzania, wakitumwagia sifa lukuki.
Tumedhihirisha
kwa vitendo kwa mara nyingine tena bila kufanya ajizi kwamba Tanzania ni kisiwa
cha amani kwa kubadilishana madaraka ya juu kabisa ya kitaifa kwa amani huku
viongozi kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya bara hili wakishuhudia kwa
nderemo na vifijo uwanjani.
Ni
utamaduni ambao nchi za wenzetu wanashindwa kuufikia na siyo kwamba hawataki
lakini wamekosa namna ya kuujenga na kuuendeleza utamaduni huu mzuri kwa kila
taifa lenye kutaka ustawi na haki kwa watu wake wote bila kubaguana.
Kama
ulivyozungumza baada ya kuapishwa kwako Rais Magufuli kwamba uchaguzi umekwisha
na Watanzania wote kwa ujumla wake wakiwemo washindani wako, na siyo wapinzani
wako katika kinyang’anyiro cha urais kwamba sasa turejee katika hali kulijenga
taifa letu baada ya kuhitimisha uchaguzi salama. Hiki ndicho kikubwa
tunachotarajia.
Kwa rais
wetu mstaafu aliyekuachia kijiti cha uongozi, Dk Jakaya Kikwete, Mungu
akuzidishie kila la heri katika maisha yako ya kustaafu baada ya kulitumikia
taifa hili, kwa umakini wa hali ya juu hadi kufikia kukabidhi jahazi hilo kwa
amani na usalama kwa mujibu wa sheria na taratibu zetu tulizojiwekea wenyewe.
Tunajisikia
fahari kuona kwamba unaungana na marais wenzako wastaafu wawili, Ali Hassan
Mwinyi na Benjamin Mkapa kuwa raia waandamizi wa nchi yetu mliosimamia kwa
umakini misingi ya kubadilishana uongozi wa ngazi ya juu wa taifa letu bila
mifarakano kwa kufuata sheria na Katiba ya nchi yetu. Mungu Ibariki Tanzania.
0 comments:
Post a Comment