MSHAMBULIAJI
wa kimataifa wa Yanga, Donald Ngoma, amesema bado hajaona mpinzani wa kumzuia
ashindwe kubeba tuzo ya Mfungaji Bora msimu huu baada ya kuizoea Ligi ya
Tanzania Bara kwa muda mfupi tangu ajiunge na timu hiyo.
Mshambuliaji
wa Stand United Elias Maguri, anaongoza mbio za ufungaji bora kwa sasa akifunga
mabao tisa huku Ngoma na Hamisi Kiiza wa Simba wakiwa nafasi ya pili kila mmoja
akiifungia timu yake mabao nane.
Ngoma
ameeleza kuwa ametoa kauli hiyo kwa sababu tayari amerudi kwenye kiwango chake
alichokizoea, hivyo hafikirii kupata upinzani utakaomfanya ashindwe kutimiza
lengo alilojiwekea.
“Sihofu
kuwa nyuma kwa bao moja kwa sababu ligi bado ni ndefu na kizuri ni kwamba
tayari nimeizoea Ligi Kuu ya Tanzania najua nifanyeje ili niweze kuipatia timu
yangu ushindi,” alisema Ngoma.
Mzimbabwe
huyo alisema anataka kuutumia msimu wake huu wa kwanza kuweka rekodi ya kuwa
mfungaji bora kwa kuwa anajua siku zijazo atakuwa na wakati mgumu, zaidi
ilivyokuwa wakati anatua kwenye Yanga kwa sababu mabeki wengi watakuwa wanajua
madhara yake.
Alisema
mbali na ubingwa, lakini pia atafurahi kuona Yanga inabeba ubingwa wa Tanzania
Bara, katika msimu wake wa kwanza akiwa na klabu hiyo kongwe nchini.
Ngoma
ametua Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, na
amejenga ushirikiano mzuri na mshambuliaji mwenzake Amissi Tambwe katika
kuifungia Yanga mabao.
0 comments:
Post a Comment