Sherehe
ya kuapishwa kwake imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya
Tanzania. Sambamba na kuapishwa Rais Magufuli, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhus Hassan pia ameapishwa.
Aidha
Rais Magufuli anashika wadhifa huo baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza
kipindi chake cha miaka 10.
SHEREHE za kumwapisha Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano wa
Tanzania, jana zilifana ambapo pamoja na wananchi wengi kujitokeza na kufurika
kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, pia marais mbalimbali wakiwemo wote wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, walihudhuria sherehe hizo.
Pamoja na kuwapo na mvua asubuhi, wananchi hao, waliwasili
uwanjani hapo mamia kwa maelfu, huku wakinyeshewa na mvua hiyo, lakini
walivumilia na kupanga mistari ya kuingia kwenye jukwaa la uwanja huo.
Majira ya saa tatu, wageni waalikwa kutoka ndani na nje
walianza kuwasili uwanjani hapo, ambapo marais watatu ambao ni Rais wa Afrika
Kusini, Jacob Zuma, Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, Rais wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi na
mkewe Isaura walikuwa wa kwanza kufika uwanjani.
Wengine ni Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Rais wa Kenya, Uhuru
Kenyatta aliyefuatana na mkewe Magreth Kenyatta, Rais wa Uganda, Yoweri
Museveni, Rais wa Zambia, Edgar Lungu na Rais mstaafu wa Comoro, Mohammed
Abdallah Sambi aliyefuatana na Spika wa Kisiwa hicho, Bourhane Hamidou.
Pamoja na viongozi hao, pia sherehe hizo zilihudhuriwa na
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn, Makamu wa Rais wa Botswana,
Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi, Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Chilima na
Naibu Waziri Mkuu wa Namibia, Marco Hausiku.
Wengine kutoka mataifa ya nje ni Naibu Waziri Mkuu wa
Swaziland Paul Dlamini, Spika wa Burundi Pie Ntavyohanyuma, Waziri wa Mambo ya
Nje wa Algeria Ramtane Lamamra na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa wa Sudan Kusini, Dk Barnaba Marial Benjamin.
Wageni wengine ni mfanyabiashara bilionea wa Afrika, Aliko
Dangote, Waziri Msaidizi wa Mambo ya Nje wa Angola, Georges Rebelo, Waziri wa
Utalii wa Oman Al Kuhuwair na mabalozi wote nchini ambao ni Balozi wa Marekani,
Uingereza, Ufaransa, Finland, Uholanzi, Ghana, Japan, Kuwait, Denmark, Norway,
Sweden na Ushelisheli.
Kwa upande wa Jumuiya za Kimataifa, pia Katibu Mkuu wa Umoja
wa Nchi za Ulaya (EU) Filbert Johnson, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) Dk Richard Sezibera na Katibu Mkuu wa Nchi za Maziwa Makuu,
Katibu Mkuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC), Stergomena Tax na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Kamlesh Sharma.
Wageni wengine kutoka nchini na viongozi wa kitaifa
waliohudhuria sherehe hizo ni marais wastaafu Benjamin Mkapa na Ali Hassan
Mwinyi. Pia mawaziri wakuu wastaafu ambao Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba,
John Malecela na Dk Salim Ahmed Salim.
0 comments:
Post a Comment