KAZI wa Dar es Salaam, Dunia Salumu maarufu kwa jina la Dk.
Manyaunyau, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela pamoja
na kulipa fidia ya Sh milioni 10 baada ya kupatikana na hatia ya
kujipatia fedha Sh milioni 29.6 kwa njia ya udanganyifu.
Manyaunyau anadaiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa
mlalamikaji, Tekra Modesta kama malipo ya kazi ya kumfufua marehemu kaka
yake aliyefahamika kwa jina moja la Modest ambaye alifariki dunia miaka
kadhaa iliyopita.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala,
Dar es Salaam, Flora Haule, alisema mtuhumiwa huyo ametiwa hatiani
baada ya ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka kujitosheleza.
“Mahakama inatoa hukumu kwa mtuhumiwa kutumikia kifungo cha miaka
mitatu jela na kulipa fidia ya Sh milioni 10 baada ya kumaliza kutumikia
kifungo chake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,”
alisema Hakimu Flora.
Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne ambao wote
waliithibitishia mahakama juu ya mtuhumiwa kujipatia kiasi hicho cha
fedha kwa njia za udanganyifu.
Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Estar Kyala, aliiambia mahakama
kuwa hakuna kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa na hivyo
kuiomba kutoa adhabu kali ili kuwa fundisho kwa wote wenye tabia kama
hizo.
Katika maelezo ya awali, ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alijipatia kiasi
hicho cha fedha kutoka kwa mlalamikaji kama malipo ya tukio la kutaka
kumfufua kaka wa mlalamikaji.
Ilielezwa kuwa mtuhumiwa alipokea fedha hizo kwa awamu mbili tofauti
ambapo awali Mei 2007 jijini Dar es Salaam alipewa kiasi cha fedha
ambacho hakikufahamika.
Mei Mosi, mwaka 2008 mtuhumiwa alipokea kiasi kingine cha fedha kama
malipo kwa ajili ya kumalizia kazi yake ya kumfufua marehemu ambaye ni
ndugu wa mlalamikaji jambo ambalo alishindwa kulitekeleza.
Manyaunyau amejizolea umaarufu mkubwa katika maeneo mengi nchini kwa
kile kinachodaiwa kuwa anao uwezo wa kutibu na kuwafichua wachawi popote
walipo sambamba na staili yake ya kunyonya damu ya paka akiwa katika
shughuli zake za uganga.
Katika tukio lililovuta wakazi wengi wa Dar es Salaam, Manyaunyau
anadaiwa kumwibua nyoka ambaye alikuwa tishio na kuzusha hofu kubwa kwa
wakazi wa maeneo ya Manzese Midizini ambapo ilidaiwa kuwa alikuwa
akiwagonga watu katika mazingira ya kutatanisha katika njia inayopita
kwenye makaburi.
Inaaminika kuwa baada ya kuitwa, Dk. Manyaunyau aliweza kumuibua
nyoka huyo na kuonekana hadharani tukio lililohisiwa kuwa ni la
kimazingara zaidi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment