LICHA ya kuachwa nyuma kwa pointi mbili na vinara Azam FC katika
msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Kocha msaidizi wa Yanga, Juma
Mwambusi, amesema licha ya ushindani mkubwa katika ligi, ana uhakika
watatetea ubingwa wao msimu huu.
Aidha, ametamba kutokana na maandalizi bora wanayoendelea nayo, haoni
kama kuna timu yenye jeuri ya kuizuia Yanga kutimiza dhamira yake.
Mwambusi, kocha wa zamani wa Mbeya City, alisema kikosi chao
kimekamilika katika kila idara na hadhani kama kuna timu
itakayowasumbua.
“Ukweli ni kwamba Yanga imetimia kwa sababu imekusanya kundi la
wachezaji wenye vipaji na ndio maana nasema sijui kama kuna timu ambayo
inaweza kutufunga…timu iko vizuri na maendeleo ya maandalizi ni mazuri
mno,” alisema Mwambusi.
Kocha huyo alisema ingawa ni muda mfupi tangu ajiunge na timu hiyo
akiwa msaidizi wa kocha raia wa Uholanzi, Hans van der Pluijm, lakini
ametambua uimara wa timu hiyo na kudai inastahili ubingwa wa Tanzania
msimu huu.
Alisema anatambua ushindani uliopo kwenye ligi ya msimu huu, lakini
hajaona timu inayoweza kuizuia Yanga kutwaa tena ubingwa. “Nimekuwa
kocha wa timu mbalimbali za Ligi Kuu ya Tanzania Bara, lakini kipindi
chote hicho sijawahi kuona Yanga bora kama ya msimu huu, ina nyota wengi
wenye vipaji halisi vya soka.
Sioni cha kuizuia Yanga kutwaa ubingwa,” alisema Mwambusi. Yanga
inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 23
huku Azam FC wakiwa ndiyo vinara kwa kujikusanyia pointi 25, timu zote
zikiwa zimecheza michezo tisa na ndizo pekee katika ligi hiyo ambazo
hazijapoteza mchezo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment