Mahakama kuu kanda ya Mwanza imetupilia mbali
mapingamizi ya kisheria yaliyowekwa na kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza na
mwanasheria mkuu wa serikali, kwamba mtoa maombi katika kesi hiyo ya madai
namba 10 ya mwaka 2015 Bw.Charles Lugiko ambaye ni baba mdogo wa marehemu
Alphonce Mawazo hana uhalali wa kisheria wa kuwasilisha maombi hayo kwa vile
yeye si baba mzazi wa marehemu.
Jaji wa mahakama kuu kanda ya Mwanza Mh. Lameck
Mlacha ametupilia mbali hoja za mawakili wa serikali Emily Kiria na Seth Mkemwa
ambao walitaka kusiwe na kesi ya msingi kwa kuwa mtoa maombi hakuwasilisha
mahakamani hapo hoja za kubishaniwa kwenye shauri hilo, huku upande wa utetezi
unaoongozwa na mawakili watatu wa chama cha demokrasia na maendeleo John
Mallya, James Ole Millya na Paul Kipeja ukijibu hoja hizo kwamba katika hatua
hiyo masuala ya kubishaniwa hayana sababu ya kuletwa kwa kuwa ni hatua ya awali
sana.
Kuhusu uhalali wa kisheria wa baba mdogo wa marehemu,
majibu yalikuwa kwamba baba mdogo kwa kuwa ndiye aliyemlea marehemu Mawazo
tangu akiwa na miezi miwili tangu kuzaliwa kwake, kwa mila za kitanzania anayo
mamlaka na uhalali wa kisheria wa kuwasilisha maombi hayo.
Mahakama imekubaliana na hoja za mawakili wa mtoa
maombi na kuamua kuruhusu kesi ya msingi kufunguliwa kama ilivyoombwa na
kutupilia mbali mapingamizi ya mlalamikiwa wa kwanza kamanda wa polisi mkoa wa
Mwanza na mwanasheria mkuu wa serikali.
Nje ya mahakama hiyo, wakili wa mlalamikaji John
Mallya amezungumza na waandishi wa habari kuelezea hatua zaidi zinazofuata
baada ya mahakama kuu kanda ya Mwanza kuruhusu kesi hiyo ambayo imevuta hisia
za mamia ya wakazi wa jiji la Mwanza kuanza kusikilizwa hapo kesho chini ya
hati ya dharura.
Uamuzi huo mdogo wa jaji wa mahakama kuu kanda ya
Mwanza Mh. Lameck Mlacha umepokelewaje na mwenyekiti wa taifa wa chama cha
demokrasia na maendeleo (Chadema) Mh.Freeman Mbowe.
0 comments:
Post a Comment