JANA katika mtandao huu tuliandika agizo la Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue la kuwataka madaktari wote nchini,kuhakikisha
wanatumia muda wao kazini na si kufanya mambo yao binafsi.
Agizo hilo ambalo alilitoa wakati anatembelea Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH) na kuwasilisha maagizo ya Rais John Magufuli, ni moja ya
maagizo muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa kutokana na unyeti wake.
Tumekuwa tukiandika malalamiko ya wananchi kuhusu matatizo
yanayosababishwa na madaktari wetu hasa pale wanapoamua kwa makusudi
kutumia vibaya muda wao. Matumizi haya mabaya ya muda huo, kumesababisha
watu kuichukia Serikali kutokana na kushindwa kupata huduma katika
hospitali zake.
Imekuwa haingii akilini kuona kwamba watu waliosomeshwa kwa kodi za
umma wa Tanzania kwa makusudi kuitumia vibaya kauli ya Serikali ya
kuwaruhusu kuwa na shughuli binafsi.
Kutokana na hali hiyo, tunapenda kumuunga mkono Katibu Mkuu kwa
maagizo yake kwa madaktari hao huku tukiwaomba wawaonee huruma
Watanzania ambao hawana fedha za kwenda katika kliniki zao.
Ni vyema katika kurejesha imani na matumaini ya wananchi wa Tanzania,
madaktari, wauguzi, wafamasia, watu wa maabara na watumishi wote wa
umma nchini kuwajibika kwa wananchi kwa kuwatumikia.
Kuwajibika kwa namna hii si kuburuzana, kwani ni ukweli kuwa upo
mkataba wa wao na mwajiri wao wa kuwatumikia wananchi katika saa
zilizokubalika. Ndio kusema madaktari wasiowajibika na kutumia muda wao
wa kazi serikalini kuhudumia wagonjwa wao binafsi hawatufai na
wanastahili kupewa adhabu ili watu waone matunda ya kodi zao.
Tunaamini wafanyakazi wote wa Afya wameona umuhimu wa agizo hilo hasa
kwa kuzingatia umuhimu wa afya za wananchi ili waweze kushiriki
kikamilifu katika kuendeleza gurudumu la maendeleo la taifa hili.
Kwa kasi tuliyo nayo ya kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati, ni
vyema watumishi wote wakashiriki kikamilifu katika kuendeleza majukumu
waliyokubali kuyabeba kwa uadilifu na umahiri mkubwa ili kila mmoja
aweze kutoa mchango wa dhati kwa maendeleo ya taifa.
Na katika hili tunamuomba Katibu Mkuu Kiongozi asichoke kufuatilia
uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma ili wananchi waone matunda ya
ulipaji kodi wao na huduma wanazostahili kuzipata kutoka serikalini.
Hata hivyo, hili lisiwe la hospitali za Serikali pekee bali kila mahali
ambapo Serikali ina mkono wake katika kuhudumia wananchi wake katika
sekta ya afya na nyinginezo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment