CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) - Zanzibar kimesema mazungumzo
yanayoendelea nchini yakiwahusisha viongozi wakuu wa kisiasa kamwe
hayajazuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu ambao matokeo yake yalifutwa na
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai
wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa. Alisema hawawezi
kukwepa mazungumzo katika kukuza demokrasia kama ni sehemu ya kuimarisha
amani na utulivu wa nchi.
Hata hivyo, alisema mazingira hayo kamwe hayawezi kuwa mbadala wa
sheria zilizopo nchini ambapo kwa upande wa ZEC imetangaza kufuta
matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu na kutaka wananchi
wajiandae kutangaziwa tarehe mpya ya Uchaguzi Mkuu.
Alisema tayari Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imetangaza kufutwa kwa
uchaguzi wa Oktoba 25 kupitia Gazeti la Serikali na hivyo kuashiria
kutoa nafasi kwa ZEC kufanya maandalizi ya uchaguzi mwingine.
Mapema, Vuai aliwataka wanaCCM Zanzibar kujiandaa na uchaguzi wa
marudio na kuepukana na propaganda zinazotolewa na wapinzani kwamba
hakuna uchaguzi mwingine. Alisema kwa upande wao wapo katika maandalizi
ya uchaguzi mwingine ikiwemo kutayarisha mawakala watakaosimamia
uchaguzi huo.
Hivi karibuni wakati akilihutubia Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano
huko Dodoma, Rais John Magufuli alisema kwa kushirikiana na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa vyama vya siasa hususan CCM na CUF
atahakikisha majaribu ya kisiasa yaliyopo yanamalizwa kwa njia ya amani
na utulivu.
Tayari mazungumzo yenye lengo la kuepusha mpasuko wa kisiasa baada ya
kfuutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 yamekuwa yakiendelea
hapa kwa nyakati tofauti yakiwahusisha wagombea urais, Dk Ali Mohamed
Shein wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF. Shein ndiye Rais wa
Zanzibar kwa sasa wakati Hamad ni Makamu wa Kwanza wa Rais.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment