Dalili hizo zinatokana na madai ya wabunge hao wa Ukawa kutaka
kupata ufafanuzi juu ya Rais Magufuli kuzindua na kulihutubia Bunge
pamoja na ujio bungeni kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein,
kutofanyiwa kazi na Spika.
Ofisi ya Spika jana ilithibitisha kupokea barua ya Kambi Rasmi ya Upinzani na kueleza kuwa inafanyiwa kazi.
Nipashe ilimuuliza Spika, Job Ndugai, kama amepokea barua hiyo na
kujibu kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi "Nimeipokea. I am Working
on it," akimaanisa anaufanyia kazi.
Jumanne ya wiki hii, Mbunge Mteule wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu, alikaririwa na Nipashe akieleza kuwa watakuja kwa muundo mpya
katika kumsusia Rais Magufuli na siyo kama ilivyozoeleka ya kutoka nje
na kwamba kuwapo Bungeni ni haki yao kwa kuwa ni wawakilishi wa wananchi
ndani ya chombo hicho.
MAOMBI YA UPINZANI
Katika barua ya Kambi hiyo iliyosainiwa na wabunge 98 wa upinzani
wa vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF, kwenda kwa Spika, imeeleza
mambo matatu ambayo yanahitaji majibu ya Spika kabla ya kufikia uamuzi
wao leo.
Mambo hayo ni mosi, haitakuwa sahihi kikanuni wala kikatiba, na
haitakubalika na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano kulihutubia Bunge na kulifungua rasmi bila uwapo ndani ya
Ukumbi wa Bunge wa Rais aliyechaguliwa kihalali na wananchi wa Zanzibar,
yaani Maalim Seif Sharrif Hamad na Makamu wake wawili wa Rais.
Pili, haitakuwa sahihi kikanuni wala kikatiba, na haitakubalika na
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Sita wa
Zanzibar, Dk. Shein, kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge kama Rais wa
Zanzibar.
"Tunataka shughuli ya ufunguzi rasmi wa Bunge usitishwe kwa sasa na
kuahirishwa hadi hapo Rais halali aliyechaguliwa na wananchi wa
Zanzibar, yaani Hamad, atakapotangazwa rasmi na kuapishwa kuwa Rais wa
Awamu ya Saba wa Zanzibar," alisema Kiongozi wa zamani wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, katika barua aliyoisoma mbele ya
waandishi wa habari juzi.
Gazeti hili lilimtafuta Mbowe, ambaye alisema yupo nje ya ofisi,
lakini hadi anahojiwa na Nipashe, hakukuwa na majibu yoyote ya barua
yao.
"Hadi sasa sijapokea majibu ya barua yetu kwa Spika, bado tuna imani kuwa itajibiwa," alisema.
Alipoulizwa ni hatua gani watachukua iwapo barua yao haitajibiwa
alijibu: " Ni mapema sana kueleza, bado nina imani barua yetu
itajibiwa," alisema.
Nipashe ilikwenda katika Ofisi ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya
zamani, na kuelezwa kuwa hakuna barua iliyopokelewa katika ofisi hiyo.
ULINZI WAIMARISHWA
Nje ya Jengo la Bunge, kuna ulinzi wa askari wenye silaha na wasio
na silaha, wakiranda randa na wengine wasio na silaha wakiwa ndani ya
viwanja vya Bunge katika maeneo yote.
Askari wa Kikosi cha Kutulinza Ghasia (FFU), walionekana wakifanya
mazoezi ya gwaride maalum litakalokaguliwa na Rais, pamoja na kuimba
Wimbo wa Taifa, ikiwa ni maandalizi ya hafla hiyo.
MAPOKEZI
Jana, watumishi wa Bunge walikuwa katika vikao vya maandalizi
mbalimbali, ikiwamo jinsi ya kupokea wageni, wakiwamo Rais wa Zanzibar,
Jaji Mkuu, Marais wastaafu, mawaziri wakuu wastaafu, kuashiria
maandalizi ya uzinduzi wa Bunge kukamilika.
UKAWA NA ZITTO
Mbowe akizungumza na Nipashe kuhusu kumkaribisha Mbunge wa Kigoma
Mjini (ACT), Zitto Kabwe, kuungana nao katika Kambi Rasmi ya Upinzani,
alisema kwa sasa hawajaanza kukaribisha mtu katika kambi hiyo.
KUUNDWA KAMBI RASMI YA UPINZANI
Mapema asubuhi, Spika Ndugai aliwataka upinzani kuunda Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni na kupeleka taarifa kwake ili itambuliwe rasmi.
Mbowe alisema wapo kwenye mchakato na wakati wowote itakamilika na kutangazwa.
SERIKALI YA KIKWETE
Wakati wa uzinduzi wa Bunge mwaka 2010, Chadema ilimsusia Rais wa
awamu ya nne, Jakaya Kikwete, kwa kutoka nje ya Bunge alipoanza
kulihutubia na kulizindua Bunge, kwa madai ya kutoitambua serikali yake
kwa maelezo kuwa wao ndiyo walikuwa washindi.
Huenda historia itajirudia leo kwa wabunge wa upinzani kutokuwapo Bungeni wakati Rais akilihutubia na kulizindua Bunge.
Katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, Dk. Magufuli
aliyekuwa mgombea wa CCM, aliibuka mshindi kwa kupata zaidi ya kura
milioni nane na kufuatiwa na Mgombea wa Chadema, Edward Lowassa,
aliyepata kura zaidi ya milioni sita.
Hata hivyo, Ukawa yenye wabunge 115 wa majimbo na viti maalum,
ilipinga matokeo hayo na Lowassa kudai alipata ushindi wa asilimia 62.2
na kueleza kuwa kulikuwa na uchakachuaji mkubwa wa matokeo.
0 comments:
Post a Comment