Image
Image

Mkwasa:Kufungwa kwa Stars sio sababu ya mimi kujiuzulu.

Kocha wa Timu ya Taifa, Taifa Stars Boniface Mkwasa ametupilia mbali hoja za kumtaka kujiuzulu nafasi hiyo kufuatia kipigo cha aibu ilichokipata Tanzania cha kufungwa mabao 7-0 na Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Russia.

Badala yake, Mkwasa amewaomba radhi Watanzania kwa kipigo hicho kinachofanya jumla ya mabao yote kuwa 9-2 baada ya sare ya 2-2 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Dar es Salaam.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkwasa alisema kwa miaka 25  aliyofundisha soka, hajawahi kuongoza timu na kufungwa idadi hiyo kubwa ya mabao.

"Matokeo haya yamenihuzunisha kupita maelezo," alisema Mkwasa.

Alisema wachezaji wake walipambana vya kutosha  kiasi cha kufika hatua ya mwisho kabisa ya uwezo wao dhidi ya timu bora Afrika.

"Kama ambavyo Mtanzania yeyote ameumizwa na matokeo haya, ndivyo mimi pia. Naomba radhi kwa matokeo haya.
"Hata kama tungefungwa, lakini siyo kwa idadi ile ya mabao, kweli hakuna anayefurahi matokeo kama haya,' alisema Mkwasa.

Alisema kufungwa kwa Stars kunatokana na ubora wa timu waliyocheza nayo. "Wachezaji wao walikuwa bora kila idara kulinganisha na wachezaji wetu.

"Hatuna wachezaji wenye kariba kama ya wapinzani wetu...wenye usumbufu na wanaojua kukaba. Hili ni tatizo kwenye timu yetu.

"Wenzetu wana wachezaji wengi wazoefu na mechi za kimataifa na wote wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi," alisema.

"Pamoja na matokeo haya mabaya, sina mpango wa kujiuzulu kama watu wanavyoshauri. Nitaendelea kuifundisha Stars na nawaomba wananchi waiunge mkono timu."

Stars sasa italazimika kusubiri harakati zingine za kucheza Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment