UTENDAJI wa Rais John Magufuli unaendelea kuwavutia watu wengi na
hatua yake ya kufuta shamrashamra za sikukuu ya Uhuru, imepongezwa kuwa
itaokoa fedha za walipa kodi, huku watendaji wa serikali wakianza
kutekeleza agizo la kufanya usafi siku hiyo ili kukabiliana na
kipindupindu.
Juzi Dk Magufuli aliwataka Watanzania popote walipo kusherehekea
sikukuu ya Uhuru, Desemba 9, 2015 kwa kufanya kazi. Kwa mujibu wa Ikulu,
maadhimisho ya Uhuru ya mwaka huu yatatumika kama kichocheo cha kujenga
tabia ya kufanya kazi (Uhuru na Kazi) nchini.
“Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa
kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini, sokoni,
viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi
kwa vitendo,” ilisema taarifa hiyo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Augustine, Profesa Mwesiga Baregu alisema siku ya Uhuru haina tatizo,
tatizo liko kwenye mfumo wa Serikali wa kuwa na matumizi makubwa ya
fedha kwenye sherehe kama hiyo na akapongeza hatua ya Rais kufuta
shamrashamra hizo.
“Rais aendelee kubana matumizi kwenye sherehe kama hizi, lakini
asiifute siku yenyewe maana iko kikatiba. Anaweza akaweka kiasi cha
fedha ambacho kinatakiwa kutumika na sio kuwaachia huru watendaji
serikalini ambako kuna mfumo mbaya wa matumizi ya fedha za umma,”
alisema Profesa Baregu. Msomi na mwanasiasa huyo wa upinzani alimuunga
mkono Rais kuondoa fedha za dhifa za Kitaifa, lakini akashauri kwamba
kwa sikukuu ya Uhuru ambayo iko kikatiba ni vyema ziruhusiwe baadhi ya
shughuli ambazo zitaienzi siku hiyo badala ya kuiondoa kabisa.
Hata hivyo, serikali katika taarifa yake ilisema kuwa sherehe hizo
zitaendelea mwaka kesho kama ilivyozoeleka na kusisitiza kwamba
haiwezekani Watanzania wakasherehekea miaka 54 ya uhuru huku wenzi wao
wakifa kwa kipindupindu. Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba
akielezea utendaji wa Dk Magufuli, alisema anaona ameanza vizuri kwa
kuwapa matumaini wananchi na akaomba asilegeze kamba kuhusu misimamo
yake.
Kibamba alishauri Dk Magufuli apewe nafasi ya kutekeleza ndoto zake
licha ya kuwa mabadiliko anayotarajia kufanya yanaweza kuchukua muda
mrefu. Hata hivyo, Kibamba alishauri rais amalizie pia mchakato wa
kuundwa kwa Katiba mpya ambao uliachwa njiani huku kukiwa na mgawanyiko
mkubwa. Pia alisema Dk Magufuli aendelee na vita dhidi ya rushwa na
ufisadi pamoja na utoaji wa haki kwa makundi ambayo yanakandamiziwa.
“Kama alivyoanza yeye mwenyewe, hata baraza lake la mawaziri ambalo
ataliunda liwe na dhamira ya dhati ya kupambana na rushwa,” alisema.
Kibamba pia alishauri Rais asiwe na msamaha kwa wote wanaokwepa kodi.
“Natamkia kila la heri katika kipindi hiki ambacho yuko kwenye mchakato
wa kuunda baraza lake la mawaziri na aendelee kuleta mageuzi makubwa
katika usimamizi wa rasilimali za umma,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Frank Tily, alisema
kuleta mageuzi sio jambo rahisi hasa katika mfumo huu ambao kuna watu
wachache wanafaidika. Akasema anatakiwa apate msaada kutoka kwa
wasaidizi wake ili afikie malengo yake. Alisema kuna haja pia ya
kuboresha maslahi ya wafanyakazi ili yakidhi wakati na wafanye kazi kwa
kasi anayotaka. Alimshauri pia Rais Magufuli kuwa na vipaumbele vichache
kama anataka kuleta maendeleo kwa haraka.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Emannuel Mallya, alisema Rais
Magufuli alipoanzia ni pazuri na akaomba na akashauri aunde mifumo
ambayo itasaidia kusukuma mbele maono yake. “Rais kwa sasa mpango wake
ni kuunda baraza la mawaziri, anaweza kuteua watu ambao watamsaidia
kujenga mifumo ambao watapanga na kutekeleza mawazo na ndoto zake za
Tanzania aitakayo,” alisema Malya.
Mjini Bukoba, siku moja baada ya agizo la Dk Magufuli, Serikali ya
Mkoa wa Kagera imeanza kutekeleza agizo hilo la usafi kwa vitendo
ikiwamo kufunga migahawa. Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella
alizindua kazi hiyo jana katika Manispaa ya Bukoba kwa kufanya usafi
katika mitaa mbalimbali na kikosi kazi cha watendaji wa Manispaa hiyo na
vyombo vya ulinzi. Mpaka jana kulikuwa na wagonjwa 26 wa kipindupindu
mkoani humo huku watu wawili wakiaminika kupoteza maisha kwa ugonjwa
huo.
Katika ‘Operesheni tokomeza kipindupindu Kagera’, Mongella alimuagiza
Ofisa Afya wa Manispaa, Ladislaus Oisso kufunga migahawa na vilabu vya
pombe za kienyeji ambavyo mazingira yake ni machafu kwa muda
usiojulikana. Alisema watakaokaidi agizo hilo, wakikamatwa watatozwa
faini ya Sh 50,000 kila mmoja. Maeneo yaliyohusika na operesheni hiyo
ambapo mkuu huyo alitembelea kwa miguu huku akishirikiana na wananchi
kufanya usafi ni kata za Bakoba, Kashai, Miembeni na Bilele zilizo
katika Manispaa ya Bukoba.
Pia aliagiza maofisa afya wote kuzibua mitaro, kuondoa na kuzoa taka
ngumu zilizopo katika maeneo mbalimbali mkoani humo. “Kipindupindu ni
ugonjwa ambao unaenea kutokana na watu kula vyakula vyenye bakteria
waliochang’anywa na kinyesi, kwa hiyo dawa ya kuzuia kipindupindu ni
kuondokana na uzembe na kufanya usafi kwa kushirikiana katika maeneo
yetu, hivyo hatuna budi kutambua kuwa wakati huu ni kuhakikisha
tunafanya usafi katika mazingira yetu, kwa hili hakuna mzaha.
Atakayekaidi atachukuliwa hatua,” alisema Mongella. Alitoa agizo kuwa
ifikapo Desemba mosi mwaka huu ugonjwa huo uwe umemalizika katika
maeneo yote ya mkoa huo na endapo katika nyumba yoyote atapatikani
mgonjwa wa kipindupindu baada ya tarehe hiyo, wahusika watafungiwa
huduma na kuwekwa katika karantini kwani sheria inayoruhusu kufanya
hivyo ipo.
Pia Mongella aliagiza kuwa maeneo yote yaliyofungwa hasa migahawa na
vilabu za pombe za kienyeji (vigata) hakuna kufunguliwa na mtu yeyote
mpaka Serikali ya Mkoa itakapojiridhisha na kutoa maelekezo upya. Aidha,
alivitaka vikosi kazi vilivyoundwa katika maeneo mbalimbali
vinavyowashirikisha polisi, mgambo na watendaji wa Manispaa kupita kwa
wananchi kuwapatia elimu juu ya suala la usafi ambalo ni agizo la Rais
Magufuli na wala siyo kwenda kwa wananchi na kuwatisha.
Aliagiza pia kwamba kila Alhamisi itakuwa siku ya usafi. Naye Mkuu wa
Wilaya ya Bukoba, Jackson Msome alisema Serikali imeshtushwa na
ongezeko la haraka la wagonjwa 10 ndani ya saa 24 ambapo Novemba 22,
mwaka huu walikuwa 16, lakini juzi wameongezeka hadi kufikia 26.
Imeandikwa na Shadrack Sagati, Dar na Angela Sebastian, Bukoba.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment