Image
Image

ACT waandaa maandamano kumuunga mkono Dk.Magufuli kwa kasi ya Utumbuaji Majipu.



CHAMA cha ACT- Wazalendo, Mkoa wa Dar es Salaam, umeandaa maandamano ya kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli katika mapambano yake dhidi ya rushwa, ufisadi na kusimamia ukusanyaji kodi kama ilani ya chama hicho inavyosema.

Katibu wa chama hicho, mkoani humo, Mhandisi Mohamed Ngulangwa, aliyasema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari na kuongeza kuwa, wamemuandikia barua Mkuu wa Mkoa huo, Said Meck Sadiki ili kumuomba ayapokee maandamano hayo ya amani.

"Tumepanga kufanya maandamano hayo Desemba 16 mwaka huu, tukianzia katika ofisi zetu za Mkoa eneo la Keko Maduka Mawili na kuishia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ilala Boma," alisema.

Alisema lengo lingine la kufanya maandamano hayo ni kumtaka Rais asimamie uongozi bora wenye lengo la kuirudisha nchi kwenye misingi iliyoasisiwa na wazee Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume.

Aliongeza kuwa, ilani ya chama chao ukurasa wa saba inaelezea ndoto ya ACT-Wazalendo ni kuona Taifa linajitegemea kiuchumi, kiutamaduni, kudumisha usawa, ustawi wa jamii, uwajibikaji, demokrasia, uongozi bora.

Mhandisi Ngulangwa alisema chama hicho kinaamini kuwa, mambo hayo yatatekelezwa vizuri kama nchi itajiwekea miiko ya uongozi kama inavyoelezwa na Azimio la Tabora lililohuishwa kutoka Azimio la Arusha.

"Lengo lingine ni kumuomba Rais ahakikishe nchi kupitia mamlaka husika, inasimamia mfumo wa matumizi ya fedha kama inavyosema katika ilani ya chama chetu ukurasa wa 23.

"Hata hivyo, yote hayatakuwa na maana kama mfumo wa fedha kupitia benki utakuwa umeshikwa na wageni kwani nchi yetu haiwezi kuendelea ikiwa benki kubwa zitakuwa zimebinafsishwa," alisema.

Alisema uanzishaji benki uliofanyika mwaka 1967 na kuundwa kwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Benki ya Nyumba na Benki ya Maendeleo Vijijini ni maamuzi ya msingi kwa maendeleo ya nchi.


Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment