Image
Image

Juhudi zinahitajika kulinda wanyama.

MOJA ya habari kubwa katika vyombo vya habari juzi na jana ni juu ya gari aina ya Mitsubishi Fuso kugonga na kuua wanyama wanane aina ya nyati katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, mkoani Morogoro.
Ajali hiyo imetokea katika barabara kuu ya Morogoro-Iringa inayokatisha kwenye hifadhi hiyo kwa ukubwa wa kilometa 50.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Dattomax Sellanyika aliyethibitisha tukio hilo, vifo vya wanyama hao ni hasara kubwa kwa hifadhi na taifa.
Alisema tukio hilo limesababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 32. Hasara hiyo ni kwa tukio moja tu, ingawa kwa mujibu taarifa za hifadhi hiyo, utafiti unaonesha zaidi ya wanyama 360 hufa kutokana na kugongwa na magari katika hifadhi ya Mikumi kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Ni sawa na wastani wa mnyama mmoja hufa kwa kugongwa kila siku katika hifadhi hiyo. Hayo yanatokea licha ya Serikali kuweka matuta na vibao vya kudhibiti mwendo kasi katika barabara kuu ya Morogoro-Iringa na kusababisha idadi ya wanyama kuendelea kupungua.
Ikumbukwe kwamba, uwepo wa wanyama katika hifadhi hii na nyingine nchini ndio unaovutia watalii kutembelea nchini, hivyo kulipatia taifa fedha za kigeni. Bila ya wanyama, ni dhahiri watalii hawawezi kusafiri umbali mrefu kuja kujionea miti na mapori tu.
Hii ina maana kwamba, kama taifa, hasa mamlaka inayosimamia Hifadhi za Taifa (TANAPA) na serikali kwa ujumla, pamoja na juhudi ilizojaribu kuchukua kulinda wanyama wetu, wana wajibu wa kuongeza elimu kwa watumiaji wa barabara hii, hususan madereva na abiria wao.
Waelimishwe umuhimu wa kutoendesha kwa kasi wakiwa hifadhini, lakini pia wazingatie masharti yote yaliyowekwa ndani ya hifadhi. Na kwamba, kama wakiendelea kuwa vichwa maji, basi sheria kali zenye kuwalazimisha kutii sheria zitapaswa kuanzishwa, ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini kubwa na ikiwezekana hata kuwatupa gerezani, huku magari yatakayosababisha ajali yakistahili nayo kuchukuliwa hatua, ikiwezekana hata kutaifishwa.
Lakini pia, kwa umbali wa kilometa 50, kamera maalumu zinaweza kuwekwa kuhakikisha mwenendo wa magari yote yanayokatisha ndani ya hifadhi yanafuatiliwa.
Aidha, kwa upande wa abiria, nao wanapaswa kuendelea kupewa elimu ya utunzaji mazingira ndani ya hifadhi, kwani kwa sasa hali ya uchafu pembezoni mwa barabara hii katika eneo ya hifadhi inaonekana kushamiri, hali ambayo inatishia usalama wa wanyama wetu.
Kama, wakikoswakoswa kuuawa kwa kugongwa na magari, basi wataangamia kwa kulishwa uchafu na sumu kutokana na vitu vinavyotupwa hovyo, hasa makopo ya soda, chupa za maji ya kunywa, karatasi za kufungashia vyakula na kadhalika.
Ndiyo maana tunashauri juhudi zifanyike kuongeza uelewa wa watumiaji wa barabara zinazopita au kuzunguka maeneo ya hifadhi zetu ili kila mmoja awe sehemu ya utunzaji wa rasilimali hizi za taifa, badala ya kushiriki kuzitokomeza kizembe.
Katika hili, kamwe hatuhitaji nguvu ya Rais Dk John Magufuli na Waziri Mkuu wake Kassim Majaliwa, bali utashi wa wenye mamlaka ya kusimamia hifadhi zetu.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment