MSHINDI wa 'Airtel Trace Music Stars’ Nalimi Mayunga
amerudi nchini kutoka Marekani alipokwenda kwa ziara ya wiki moja kwa ajili ya
kurekodi video yake na kupata mafunzo kutoka kwa mwanamuziki nguli Akon.
Nalimi Mayunga alisema hii imekuwa nafasi ya pekee
maishani mwake na anapenda kuwashukuru sana Aitel na Trace kwa kumpatia fursa
hiyo.
"Nimefurahia muda niliokaa Marekani na kupata
wakati mzuri wa kumtembelea Akon nyumbani kwake na kurekodi video na kupata
mafunzo ya muziki,” alisema.
Nalimi aliongeza kwa kusema fursa hiyo imempa mwanga
zaidi katika namna ya kufikiri na kujipanga, ili kuzifikia ndoto zake katika
tasnia ya muziki.
"Nimejifunza mambo mengi sana kupitia mafunzo
niliyopata kutoka kwa Akon ikiwemo jinsi ya kukabili jukwaaa, namna ya kuchezea
sauti yangu, mafunzo ya sauti, namna ya kuandika na kutunga nyimbo na jinsi ya
kuinua muziki wangu na kukuza kipaji changu kwa ujumla."
Nalimi aliyejawa furaha pia alieeleza shauku
aliyonayo ya kutoa kibao hicho kwa kushirikiana na Akon na kusema kwamba
kitafungua milangoyake katika ulimwengu wa muziki, kwani amepata nafasi ya
kuingia na kurekodi wimbo wake kwenye studio ya Universal Hollywood yenye vifaa
vya kisasa na vyenye teknologia ya juu.
"Nina uhakika video yangu itakuwa moja kati ya
video bora za muziki sokoni na hivyo nawashurukuru sana mashabiki wangu,
Watanzania kwa ujumla kwa kunipigia kura na kuniwezesha kufika hapa nilipo
leo."
Akieleza zaidi kuhusu safari ya Mayunga, Mkurugenzi
wa Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Singano Malya alisema 'Tunafurahi kuwa
sehemu ya kubadilisha maisha ya vijana wengi akiwemo Nalimi Mayunga. Tunaamini
Mayunga atakuwa ni mfano utakaowavutia vijana wengi kuzifikia ndoto zao.
Tunapenda kuwahamasisha vijana wengi zaidi kushiriki katika program zetu nyingi
zenye lengo la kuwawezesha kufikia malengo yako kama vile Airtel Fursa, Airtel
Rising Stars, Airtel Trace Music Stars na nyingine nyingi.”
Msimu wa pili wa shindano kubwa la muziki la Afrika
la Airtel Trace Music Stars mwaka 2016 linategemea kuzinduliwa rasmi mwanzoni
mwa Januari, mwakani na wanatoa wito kwa vijana wengi kushiriki pindi shindano
hilo litakapotangazwa rasmi.
0 comments:
Post a Comment