Bohari Kuu ya Dawa (MSD), imeanza kufungua maduka ya dawa katika hospitali za serikali kwenye mikoa mbalimbali. Hatua ya MSD ya kufungua maduka ya dawa katika hospitali za serikali lengo lake kubwa ni kurahisisha upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa pamoja na kudhibiti vitendo vya wizi wa dawa katika hospitali za umma na kutumika katika maduka ya watu binafsi kwenye maeneo ya hospitali hizo.
Zimekuwapo tuhuma nyingi kwamba baadhi ya watumishi katika
hospitali za umma wamekuwa wakiiba dawa na kuuzwa katika maduka ya dawa
yaliyoko katika maeneo ya hospitali za serikali huku wagongwa waliolazwa
wakikosa dawa. Hii ni kero kubwa na ya muda mrefu ambayo kila mmoja
angependa kuona inakomeshwa.
Uamuzi wa MSD wa kufungua maduka yake ya dawa katika maeneo ya
hospitali za umma ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais John
Magufuli, baada ya kubaini kuwa maduka kadhaa ya dawa ya watu binafsi
yaliyoko kwenye hospitali za umma yanatumika kuuza dawa zinazoibwa
katika hospitali za serikali na kuwalazimisha wagonjwa kuzinunua dawa
hizo katika maduka binafsi, tena kwa gharama kubwa.
Rais Magufuli aliizungumzia sana kero hiyo katika mikutano yake ya
kampeni za Uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kuahidi kwamba akichaguliwa
ataikomesha.
Katika utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli, MSD imeshafungua duka
la dawa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambalo limeanza
kufanya kazi rasmi huku ikijiandaa kufungua maduka zaidi katika
hospitali nyingine za serikali nchini. MSD imesema iko mbioni kufungua
maduka mengine mawili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya na ya
Mount Meru mkoani Arusha.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu, baada ya
kukamilisha duka la Muhimbili, watahamia katika mikoa hiyo miwili.
Tunaipongeza MSD kwa kutekeleza haraka agizo la mkuu wa nchi, ambalo
lengo lake ni kuhakikisha huduma za afya kwa Watanzania wengi ambao ni
maskini zinaboreshwa ikiwamo kupata dawa za uhakika na kwa gharama
nafuu. Hata hivyo, tunashauri kwamba MSD isijikite kufungua maduka ya
dawa tu, bali kuhakikisha kuwa dawa za kutosha zinapelekwa katika maduka
hayo sambamba na vifaa tiba.
Hakutakuwa na maana kama yatafunguliwa maduka mengi ya dawa kwenye
hospitali za serikali bila kuwapo dawa za kutosha pamoja na vifaa tiba
kwa ajili ya wagonjwa.
Jambo la kutia moyo ni kuwa mahitaji ya dawa na vifaa tiba ni
makubwa, hivyo MSD ikifungua maduka katika hospitali zote za serikali
zitanunuliwa.
Tunafahamu kuwa kutakuwapo na changamoto kadhaa katika utekelezaji
wa agizo la Rais Magufuli, lakini tunaishauri MSD ihakikishe kwamba
dawa, vifaa tiba vya kutosha vinapelekwa katika maduka hayo na kuuzwa
kwa gharama nafuu ili wagonjwa wazimudu.
Bwanakunu anaelezea baadhi ya changamoto wakazokabiliana nazo kuwa
kuna uwezekano wa kuchelewesha ukamilikaji kwa sababu kazi ya ukarabati
wa maduka hayo inagharimu kiasi kikubwa cha fedha.
Ni matarajio yetu kuwa MSD italitekeleza agizo hilo kwa wakati
mwafaka na kwa tija na ufanisi, lakini ihakikishe pia inapeleka dawa za
kutosha kwenye maduka hayo.
Tunatambua kuwa MSD inaidai serikali deni kubwa la muda mrefu,
lakini kasi kubwa ya utekelezaji wa majukumu ambayo imeonyeshwa na
serikali ya Magufuli, tunaamini deni hilo litalipwa.
0 comments:
Post a Comment