WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia
na Mafunzo ya Ufundi, Dk Joyce Ndalichako, amesema atafuatilia shule za
Serikali ili kujua sababu za kufanya vibaya katika mitihani yao. Dk Ndalichako
ambaye aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), amesema hayo
jana baada ya kuapishwa na Rais John Magufuli, kushika wadhifa huo.
“Kwa kuwa lengo langu ni kuona elimu
bora inatolewa, nitafuatilia kujua sababu ya shule maalumu za Serikali kushuka
kiwango chake katika ufaulu wa mitihani,” alisema. Kwa mujibu wa Dk Ndalichako,
shule hizo za Serikali hasa za vipaji maalum, ndizo awali kila mwanafunzi
alipenda kwenda kusoma tofauti na sasa ndio maana anataka kujua kulikoni.
Shule hizo ni pamoja na Mzumbe,
Ilboru, Tabora Wavulana, Tabora Wasichana, Kilakala na Msalato. Ada holela,
kukaa chini Kuhusu upandaji holela wa ada za shule binafsi, Dk Ndalichako
alisema atapambana na vyuo vikuu na shule binafsi, zinazofanya ujanjaujanja wa
kupandisha ada tofauti na ile iliyoandikwa kwenye barua za kuwaita wanafunzi,
jambo linalosababisha usumbufu kwa wazazi.
Alisema lengo lake ni kuhakikisha
Tanzania inatoa elimu bora kwa wahitimu wa vyuoni na sekondari,
itakayowawezesha kukidhi soko la ajira la kimataifa. Pamoja na ubora huo, Dk
Ndalichako alisema ataangalia uwepo wa miundombinu kwa wanafunzi wa kuanzia
shule ya msingi na sekondari, ambako alikiri kuwa baadhi ya wanafunzi wanaketi
chini na wengine wana matatizo ya mashimo ya vyoo.
“Inakuwaje shule yenye maelfu ya
wanafunzi watumie shimo moja la choo, haya na mambo mengine yanakwaza wanafunzi
wasipende shule na wengine wakatize masomo yao. “Tunataka kuandaa mwanasayansi,
hivi kweli mwanafunzi anayeketi chini anaweza kuwa mtaalamu mzuri wa sayansi?
Ni lazima tuwezeshe shule zetu ziwe na miundombinu rafiki kwa wanafunzi,”
alisema Dk Ndalichako.
Pia alisema atashughulika na tatizo la
baadhi ya vyuo kutoa kozi zinazoenda kinyume na ithibati walizopewa na mamlaka
za elimu, jambo linalofanya wanafunzi wanaosoma kwenye vyuo hivyo kutotambuliwa
na waajiri.
Profesa Mbarawa Kwa upande wake,
Profesa Makame Mbarawa, ambaye amevaa viatu vya Dk Magufuli kwa kuwa Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, alimshukuru Rais kwa kumwamini ili avae viatu
vyake.
Pia, alikiri hatakuwa kama alivyokuwa
mtangulizi wake kwa sababu mbalimbali, ikiwemo uzoefu wa kazi ndani ya wizara
husika. “Kiukweli mtangulizi wangu ni mtaalamu zaidi katika wizara hii na
alikaa muda mrefu, hivyo siamini kama nitaweza kuwa kama yeye, ila nitajifunza
kwake zaidi na ninategemea ushauri wake katika kutekeleza majukumu yangu
mapya,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema ameingia kwenye wizara hiyo,
akiamini kuwa nchi bila kuwa na miundombinu madhubuti, haiwezi kufikia malengo
yake, hivyo mkakati wa wizara yake ni kuunganisha nchi kwa barabara za lami
kati ya makao makuu ya wilaya na wilaya, ili kufikia Dira ya Taifa ya mwaka
2025.
Alisema anatambua kwamba kuna miradi
ya barabara zenye urefu wa kilometa 3,000, ambazo tayari makandarasi wanaendelea
na ujenzi, hivyo atazisimamia ili zikamilike kwa wakati. Mbali na hiyo, pia
alisema kuna barabara nyingine zenye urefu wa kilometa 4,600, ambazo
makandarasi wamepatikana na sasa ujenzi wake unasubiri kuanza; “Hizo nazo
naahidi kuwa tutazijenga ndani ya miaka mitano,” alisema.
Alisema miradi mingine ambayo Wizara
ya Ujenzi chini ya Dk Magufuli imejipangia kuijenga miaka ijayo, yeye ataenda
kusimamia pamoja na sera za chama kuhakikisha kuwa ndoto ya ujenzi wa barabara
hizo pia unakamilika.
Kwa upande wa reli, alisema kumekuwapo
mpango wa kujenga Reli ya Kati ili iwe ya kisasa zaidi kuliko ilivyo sasa na
alisema anaamini Serikali imefikia pazuri na muda wowote ujenzi wake utaanza.
“Muda umefika sasa wa reli hiyo ianze
kujengwa na Watanzania watarajie kuiona ili mizigo isafirishwe kwa treni na
badala ya barabara, binafsi naamini kipindi hiki reli itaanza kujengwa,”
alisema Profesa Mbarawa.
Kwa upande wa sekta ya uchukuzi,
alisema kuna fursa nyingi ambazo Taifa likitumia vizuri, itakuwa rahisi nchi
kutekeleza lengo lake la kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
0 comments:
Post a Comment