Kutolewa kwa Stars kunaandika rekodi mpya kwa Stars kushiriki
michuano hiyo kwa mara ya tatu mfululizo bila kutwaa kombe hilo. Mara ya
mwisho Stars kutwaa kombe hilo ilikuwa 2010 wakati michuano hiyo
ilipofanyika jijini Dar es Salaam.
Mwaka 2011 Uganda walikuwa mabingwa na walitetea ubingwa wao mwaka
uliofuata, yaani 2012, kabla ya Kenya kuwapiku 2013 Kenya. Michuano hiyo
haikufanyika mwaka jana kutokana na hali mbaya ya kifedha iliyokuwa
inawakabili waandaji.
DHARAU
Kili Stars imeshindwa kufanya vyema mwaka huu katika michuano hiyo
kutokana na wachezaji wa timu hiyo kuamini kuwa timu hiyo ni bora kuliko
timu zote na tayari walikuwa wamejijengea fikra kuwa hakuna wa
'kuwagusa mpaka fainali'.
Fikra hizo zilikuwa ni nzuri, lakini walihitaji kujituma na kufanya
kazi bila ya kuangalia wanacheza na timu kibonde au timu ngumu. Stars
ilitolewa dhidi ya Ethiopia ambayo ilikuwa ikicheza soka lisiloeleweka
kimfumo.
PENGO LA AISHI MANULA
Kukosekana kwa Aishi Manula (alikuwa na rekodi ya kadi za njano)
kwenye kikosi cha Stars katika mechi yao iliyowang'oa ya robo-fainali
dhidi ya Ethiopia, kuliigharimu timu hiyo ya Bara kwani kipa Said
Mohamed 'Nduda' alionekana kukosa uzoefu kwenye michuano hii, ikiwa ni
mechi yake vya kwanza kwenye kikosi hicho mwaka huu.
Presha ilionekana kuwa kubwa kwake hasa wakati wa penalti, akifungwa mikwaju yote minne iliyopigwa na nyota wanne wa Ethiopia.
Bila shaka, kipa mzoefu wa michuano ya kimataifa, Ally Mustafa 'Barthez' aliyekuwa benchi Jumatatu
angekuwa chaguo zuri kwenye hatua ya matuta kutokana na ukweli kwamba Nduda tayari alikuwa na
presha ya kufungwa goli ndani ya dakika 90 za mchezo.
WASHAMBULIAJI BUTU
Kocha wa Kili Stars, Abdallah 'King' Kibadeni alikuwa akiwatumia zaidi washambuliaji John Bocco, Elias
Maguli na Malimi Busungu kwenye eneo la kati la ushambuliaji,
lakini kocha huyo anadai mastraika hao walikosa nafasi nyingi
ukilinganisha na matokeo waliyokuwa wakipata.
Nipashe iliyopiga kambi jijini hapa mwanzo-mwisho kufuatlkia
michuano hiyo mwaka huu, ilishuhudia nafasi mbili hadi tatu zikipotezwa
'kizembe' na mastraika Maguli na Bocco katika kila mechi waliyocheza.
VURUGU ZILIWATOA MCHEZO
Penalti iliyosababishwa na beki wa pembeni kulia Shomary Kapombe na
kuzaa bao la kusawazisha la Ethiopia katika dakika ya 56 ilionekana
kuwatoa mchezoni nyota wengi wa Stars.
Wengi wao walionekana kukosa imani na mwamuzi kiasi cha kuanzisha
vurugu zilizosimamisha mchezo kwa dakika tatu huku baadhi ya wachezaji
akiwamo nahodha Bocco wakionywa kwa kadi za njano.
Vurugu zilipomalizika wachezaji wengi wa Stars walionekana kupunguza kasi na kukata tamaa ya kusaka ushindi.
KUVIMBA KICHWA
Tatizo kubwa la Stars ya Chalenji 2015 lilikuwa wachezaji wake
kujiamini kupita kiasi, walijua fika wangeitoa Ethiopia na kwenye
michezo yote miwili dhidi ya timu hiyo (hatua ya makundi na
robo-fainali)
walionekana kutopania ushindi.
Mabeki wa pembeni Mohamed Hussein 'Tshabalala' na Hassan Kessy
walionekana kupoteza muda bila sababu kuntu katika mechi ya
robo-fainali. Pia wachezaji walikuwa wakiweka 'njonjo' nyingi wakati
timu ilikuwa ikihitaji zaidi mabao kuliko maonyesho ya jinsi ya
kuuchezea mpira.
KELELE ZA MASHABIKI
Kelele za mashabiki wa Ethiopia ambao walijitokeza kuishangilia
timu hiyo pia zilionekana kuchangia kuivuruga Stars. Licha ya kuwa na
nyota wengi wenye uzoefu wa mechi za kiimataifa, tmu hiyo ilikuwa
inacheza kwa presha, hasa baada ya wenyeji kusawazisha.
Hali hiyo pamoja na vurugu na uamuzi ya mwamuzi kutoa penalti
ambayo nyota wengi wa Stars waliona ilikuwa na utata, vilichangia kwa
kiasi kikubwa kuivuruga timu yao kumalizia dakika 36 za mwisho ambazo
ilishindwa kutengeneza mashambulizi ya maana.
Wachezaji na hata benchi la ufundi la Stars lilikuwa linamsakama
refa kwa madai kwamba alichezesha mechi kwa maagizo ya waandaaji
kuhakikisha wenyeji Ethiopia inasonga mbele ili kuchangamsha michuano.
Jambo pekee la kujivunia ni kwamba Stars imeaga mashindano ikiwa
haijapoteza mchezo hata mmoja ndani ya dakika 90. Kwenye hatua ya
makundi timu hiyo ilipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Somalia,
kisha ikaifunga Rwanda 2-1 na kutoa sare ya 1-1 dhidi ya Ethiopia
kabla ya kung'olewa kwa matuta 4-3 dhidi ya wenyeji hao baada ya sare ya
1-1 tena ndani ya dakika 90.
'SUB' 3 DAKIKA 360
Ni straika Malimi Busungu na kiungo Jonas Mkude pekee ambao
walitokea benchi la Stars kwenye michezo yote minne. Stars ndiyo timu
iliyofanya mabadiliko 'kiduchu' zaidi kwenye michuano hiyo mwaka huu
licha ya kanuni za mashindano kuruhusu kubadili wachezaji watatu katika
kila mchezo.
Kibadeni alimwingiza Busungu kwenye mchezo dhidi ya Somalia kuziba
nafasi ya winga Simon Msuva. Kwenye mchezo dhidi ya Rwanda pia alimtoa
kiungo Himid Mao na kumuingiza Jonas Mkude wakati kwenye mchezo wa tatu
wa makundi kocha huyo hakufanya mabadiliko yoyote.
Katika mechi ya robo-fainali, kocha huyo wa zamani wa Simba na Ashanti United, alimtoa winga Deus Kaseke na kumwingiza Busungu.
MAGOLI NANE
Stars imefanikiwa kufunga jumla ya mabao nane kwenye michuano hiyo
ikiwa ni wastani wa kufunga mabao mawili katika kila mchezo huku
ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu.
Mabao ya timu hiyo yalifungwa na John Bocco (3), Elias Maguli (2), Simon Msuva (2) na Said Ndemla aliyetupia moja.
PASI ZA MWISHO
Katika mechi zote nne mastraika wa Stars walitengenezewa jumla ya
mabao sita huku mabao mawili yakitokana penalti na lingine mpira wa
adhabu.
Winga Msuva ameongoza kwa kutoa krosi tatu zilizozaa mabao, wakati
beki wa pembeni kushoto Tshabalala alitoa krosi mbili zilizozaa mabao
huku Maguli akipiga pasi moja iliyozaa bao.
NIDHAMU
Nidhamu ya nje ya uwanja kwa wachezaji wa Stars ilikuwa ni nzuri
kwani muda wote walikuwa kambini na walikuwa wakifuata kwa muda kile
walichotakiwa kukifanya.
Wachezaji wa Stars walipata jumla ya kadi nane za njano kwenye
mechi zote nne walizocheza. Katika mechi ya kwanza dhidi ya Somalia
hakukuwa na kadi yoyote, mchezo dhidi ya Rwanda, Kapombe alionywa kwa
kadi, mchezo wa tatu dhidi ya Ethiopia, kipa Manula, beki Kessy, kiungo
Mao na winga Msuva
walionywa kwa kadi za njano.
0 comments:
Post a Comment